Wednesday, May 11, 2016

SERENGETI BOYS YAPAA LEO KWENDA GOA, INDIA, LIGI DARAJA LA PILI IMEANZA

Timu ya soka ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama jina la Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka leo Jumatano Mei 11, 2016 saa 10.00 jioni kwenda Goa, India kwa ajili michuano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).
Timu hiyo ambayo juzi iliagwa rasmi na kukabidhiwa bendera na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT), Dioniz Malinzi inaondoka na matumaini ya kufanya vema kwenye michuano hiyo hasa wakichukulia kwamba michuano hiyo inakwenda kuwaweka sawa na maandalizi ya kuivaa Shelisheli katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani Afrika ambako mchezo wa kwanza utakaofanyika Juni 25 wakati ule marudio utafanyika Julai 2, 2016.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime amesema wametiwa nguvu na waratibu wa michuano hiyo wakiwamo Balozi wa India nchini, Sandeep Arya na Naibu Balozi, Robert Shetkintong hivyo wanakwenda kujitahidi kufanya vema katika kila mchezo ili kurejea nyumbani na kikombe saa 1.15 jioni siku ya Mei 26, 2016.

Shime anajivunia kikosi cha wachezaji 22 anachoondoka nacho kinachoundwa na makipa, Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.

Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng'anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.

Maofisa watakaosafiri na timu hiyo ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami, Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa, Edward Edward.

Michuano hiyo itakayopigwa kwa mfumo wa ligi kwa timu tano kucheza mechi nne, inatarajiwa kuanza Alhamisi Mei 12, 2016 na kwamba AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.

Tayari Serengeti Boys imecheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa mpaka sasa, mmoja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya vijana wa Misri (The Pharaohs) na kupata matokeo mazuri na tangu Aprili, 2016 iliweka kambi katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa na michuano hiyo chini ya Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa.

Tangu kuanza kwa maendeleo ya soka la vijana, mashindano hayo yamekuja wakati mwafaka kuwa ni hatua kubwa ya maendeleo ya soka Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa haijawahi kutokea timu kama hiyo ikateuliwa kushiriki michezo ya shirikisho kabla ya fainali za Kombe la Dunia kwa vijana.

“Kwa kawaida au tuseme kwa mujibu wa ratiba za fainali kubwa zinazofanyika katika nchi fulani, mwaka mmoja kabla huandaliwa mashindano ya shirikisho kama haya. India mwakani wana mashindano makubwa, fainali za Kombe la Dunia kwa timu za vijana na hivyo ni wameandaa mashindano ya shirikisho ambayo Tanzania, Malaysia, Korea Kusini, Marekani na India wenyewe tumealiwa,” amesema na kuongeza kuwa Serengeti Boys inatarajiwa kusafiri kwenda India Jumatano Mei 11, mwaka huu.

Ratiba
Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.

LIGI DARAJA LA PILI
Ligi Daraja la Pili (SDL) Tanzania Bara imeanza kuchezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam kwa kuzikutanisha timu nne zinazowania kupanda kucheza Daraja la Kwanza (FDL), msimu wa 2016/17.

Timu hizo zilizoanza kuchuana Mei 11, zitacheza ligi hiyo hadi Mei 18, mwaka huu inazikutanisha Mvuvumwa ya Kigoma, Abajalo ya Dar es Salaam, Pamba ya Mwanza na The Mighty Elephant na mbili kati ya hizo zitakazofanya vema ndizo zitakazopanda daraja.

Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inasema michezo hiyo zinazopigwa kuanzia saa 10.00 jioni, kiingilio chake kimepangwa kuwa Sh 1,000.

Ratiba ya ligi hiyo inaonesha;
Leo Mei 11, 2016 Abajalo v Mvuvumwa
Mei 12, 2016 Pamba v The Mighty Elephant
Mei 14, 2016 The Mighty Elephant v Mvuvumwa
Mei 15, 2016 Abajalo v Pamba
Mei 17, 2016 Mvuvumwa v Pamba
Mei 18, 2016 The Mighty Elephant v Abajalo

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Nassibu Mabrouk ametowa wito kwa wakazi wa Mwanza kuichangia timu ya Pamba maarufu kama TP Lindanda iliyoko Dar es Salaam kwa sasa, ili iweze kufanya vema.