Tuesday, June 28, 2016

CAF CC: LEO NI YANGA DHIDI YA TP MAZEMBE TAIFA NANI KUIBUKA KIDEDEA?

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, Leo kibarua kigumu kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam watakapocheza na Miamba ya Afrika TP Mazembe ya Congo DR ikiwa ni Mechi ya Pili ya Kundi A la Mashindano ya Klabu Barani Afrika ya KOMBE LA SHIRIKISHO, CAF CC.
Mechi ya kwanza Yanga walianza Ugenini huko Algeria na kufungwa 1-0 na MO Bejaia wakati TP Mazembe, waliowahi kutwaa Ubingwa wa Afrika mara 5, walianzia kwao Lubumbashi kwa kuitwanga Medeama ya Ghana 3-1. Mara baada ya kipigo cha Bejaia, Yanga walipitia Uturuki ambako walipiga Kambi ya muda wakijisuka upya na kurejea Dar es Salaam Juzi.
Nao TP Mazembe walitua Dar es Salaam Jumapili wakiwa na Kikosi cha Wachezaji 18 na mmoja wao ni Straika wa Timu ya Taifa ya Tanzania Thomas Ulimwengu.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, amesema Kikosi chao kiko imara na kitapigania ushindi ili kujiweka vizurikwenye Kundi A.
Mechi nyingine ya Kundi A ni Jumatano Juni 29 wakati Medeama wakiwa kwao Ghana kucheza na MO Bejaia ya Algeria.