Monday, June 13, 2016

COPA AMERICA CENTENARIO: GOLI LA UTATA LAITUPA BRAZIL NJE!

BRAZIL wametupwa nje ya Mashindano ya Copa América Centenario walipofungwa 1-0 kwa Bao la utata mkubwa na Peru kwenye Mechi yao ya mwisho ya Kundi B iliyochezwa huko Gillette Stadium, Foxboro, Massachusetts, USA.
Toka Kundi B, Peru na Ecuador, ambao Asubuhi hii waliitwanga Haiti 4-0, wametinga Robo Fainali.
Hii imekuwa ni mara ya kwanza tangu 1987 kwa Brazil kushindwa kuvuka hatua ya Makundi ya Mashindano haya na safari hii Bao la utata mkubwa ndio liliwaua wakati wakihitaji Sare tu ili wasonge.

Bao hilo la Peru lilifungwa Dakika ya 75 kufuatia Krosi Andy Polo kutumbukizwa wavuni na Raul Ruidiaz na marudio kuonyesha waziwazi Mfungaji alitumia mkono kufunga.

Awali Refa Andres Cunha alilikubali Bao hilo na kisha kusita na kutumia Dakika zifikazo 5 akishauriana na Msaidizi wake Mshika Kibendera huku Brazil wakilalamika sana.

Kwenye Mechi ya Ecuador waliyoishinda Haiti 4-0, Bao zao zilifungwa na Enner Valencia, Dakika ya 11, Jaime Ayovi, 20, Cristian Noboa, 57, na Luis Antonio Valencia, 78.

Kwenye Robo Fainali, Wenyeji USA watacheza na Ecuador na Peru kuivaa Colombia.