Saturday, June 11, 2016

DAVID DE GEA APINGA “UZUSHI KASHFA YA NGONO”, ABAKI KAMBINI NA SPAIN!

KIPA wa Manchester United David de Gea ambae sasa yupo kwenye Kambi ya Timu ya Taifa ya Spain ikijitayarisha kucheza Fainali za EURO 2016 amekanusha madai kwamba yeye anahusika kwenye kashfa ya ngono baada ya kudaiwa Jina lake kutajwa kwenye Kesi iliyopo Mahakamani na kwamba ametimuliwa Kikosini.

Akiongea Jana na Wanahabari kwenye Hoteli ambayo Kikosi cha Spain kimepiga Kambi huko kwenye Kisiwa cha Ile de Re, De Gea alikanusha kuhusika kwake na kusisitiza yupo makini kwa kuichezea Spain kwenye EURO 2016 na hajafukuzwa Kikosini kama uvumi ulivyozagaa.

Jana Jioni Vyombo vya Habari vya Spain vilitapakaza habari kuwa De Gea alitajwa Mahakamani na Shahidi mmoja kwenye Kesi inayohusisha Watu wengine kwamba yeye ndie aliekamilisha na kulipia ili Wachezaji Wawili wa Kikosi cha Spain cha U-21 wakutane na Wanawake Wawili kwenye Hoteli moja huko Madrid, Spain Mwaka 2012.

Lakini, akisisitiza kuwa habari hizo ni ‘uongo’, De Gea alieleza: “Nimeshangazwa mno na habari hizi. Nataka nizipinge. Ni uongo na ni mambo ya uongo.”

Aliongeza: “Sijui haya yametoka wapi na yamefikaje kwa Wanahabari. Ni njia ya kumpaka Mtu matope. Nilichofanya kwanza ni kuongea na Familia yangu ili wasipate wasiwasi. Lakini wananijua mimi. Najua nilichofanya maishani mwangu kwa hiyo nipo mtulivu. Hili linanipa sababu kubwa kubakia Spain nikiwa pamoja na Wachezaji wenzangu.”

Spain, ambao ndio Mabingwa Watetezi wa Ulaya, wataanza utetezi wao na Czech Republic huko Stadium Municipal Mjini Toulouse hapo Jumatatu Juni 13 ikiwa ni Mechi ya Kundi D ambalo Timu nyingine ni Turkey na Croatia.