Thursday, June 30, 2016

ENGLAND – MSAKO MENEJA MPYA: SOUTHGATE HUENDA AKAKAIMU KWA MUDA!

ENGLAND inatafakari uwezekano wa kumteua Gareth Southgate awe Meneja wa Muda wa England kufuatia kuondoka kwa Roy Hodgson mara baada ya England kutupwa nje ya EURO 2016 kwenye Hatua ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16 na Iceland huko France.
Southgate, ambae sasa ndie Bosi wa Timu ya Taifa ya England ya Vijana chini ya Miaka 21, U-21, anaweza kuteuliwa ili kuisimamia Timu hiyo ikianza kampeni yake ili kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.

Wakiongea na Wanahabari, Mtendaji Mkuu wa FA, Chama cha Soka England, Martin Glenn, akiwa pamoja na Roy Hodgson hapo Jana, alidokeza kuwa kumsaka Meneja mpya kunaweza kuchukua Miezi kadhaa.

Hivi sasa huko England Majina kadhaa yamekuwa yakitajwatajwa n ahata Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ambae sasa yuko kwenye Mwaka wa mwisho wa Mkataba wake na Arsenal, anatajwa mno kufaa kuwa Meneja mpya wa England.

Alipoulizwa moja kwa moja kama Southgate anaweza kuiongoza Timu kwa ajili ya Mechi yao ya kwanza ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za 2018 hapo Septemba dhidi ya Slovakia, Glenn alijibu: “Tutaona. Tunataka tumpate kabla ya hiyo michujo ya Kombe la Dunia lakini kama hatukumpata tuna mipango ya muda. Hatuzungumzii Majina lakini hilo lake lipo wazi!”

Mchakato wa kumpata Meneja mpya wa England utasimamiwa na Glenn mwenyewe pamoja na Mjumbe wa Bodi ya FA, David Gill, na Mkurugenzi wa Ufundi wa FA, Dan Ashworth.