Saturday, June 11, 2016

EURO 2016 – FAINALI: LEO ENGLAND INAANZA NA RUSSIA KUMALIZA UKAME WAKE WA MIAKA 50!

Jumamosi Juni 11
KUNDI A
, Albania v Switzerland (1700, Stade Bollaert-Delelis, Lens)
KUNDI B, Wales v Slovakia (2000, Stade de Bordeaux)
KUNDI B, England v Russia (2300, Stade Velodrome, Marseille)

LEO, Euro 2016, Mashindano ya Mataifa ya Ulaya, itaendelea kwa Mechi 3 Makundi A na B baada ya Mashindano haya kuanza rasmi Jana kwa Mechi ya Kundi A iliyochezwa Stade de France Mjini Paris na Wenyeji France kuibuka na ushindi wa Bao 2-1.

Leo ipo Mechi 1 ya Kundi A kati ya Albania na Switzerland na mbili za Kundi B kati ya Wales na Slovakia na Mechi kali kati ya England na Russia itakayochezwa huko Stade Velodrome huko Mjini Marseille Nchini France.

IFUATAYO NI TAARIFA YA MECHI ENGLAND v RUSSIA:
Hali za Timu

Kwa Kikosi cha England, chini ya Kocha Roy Hodgso, kilikuwa na wasiwasi kuhusu Chris Smalling, Gary Cahill na Ryan Bertrand baada ya kupata maumivu lakini wote wametangazwa kuwa ni fiti.

Kwa upande wa Russia, chini ya Kocha Leonid Slutsky mwenye Miaka 45 ambayo inamfanya awe Kocha Kijana kupita yeyote kwenye EURO 2016, wao walipata pigo baada ya kuwasilisha UEFA Majina 23 ya Kikosi chao na kisha Alan Dzagoev na Igor Denisov kuumia na kuondoka Kikosini.

Pia Russia itamkosa Mchezaji wa zamani wa Chelsea Yuri Zhirkov mwenye maumivu ya Kifundo cha Mguu.

Tathmini ya Mechi
England wapo kwenye Fainali za Mashindano makubwa wakiwa na hamu kubwa ya kumaliza ukame wao wa Miaka 50 ya kutwaa Taji ambalo la mwisho kwao ni Kombe la Dunia walipolibeba kwao Wembley, London Mwaka 1966.

Safari hii wana Kikosi kikiwa na Vijana wengi wakiongozwa na Kepteni wao mkongwe wa Timu Wayne Rooney ambae ndie Mfungaji Bora wa England katika Historia yao.

Kikosi hiki kinatinga EURO 2016 kikiwa Timu pekee iliyoshinda Mechi zao zote za Makundi ya Mashindano hayo.

Kwenye EURO 2012, England ilitoka Sare 1-1 na France katika Mechi yake ya ufunguzi.

Kwa Russia, hii Mechi hii na Mashindano haya ni mazoezi muhimu kwa Uenyeji wao wa Mashindano makubwa ya FIFA ya Kombe la Shirikisho Mwakani na Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018.

Kama ilivyokuwa kwa England, Russia nayo ilitupwa nje ya Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil kwenye Hatua za Makundi.

Habari zilizovuja na kupaishwa na Wanahabari wa England ni kuwa Leo Kocha Hodgson atawapiga Benchi Jamie Vardy na James Milner na kuwaanzisha Wayne Roone, Harry Kane pamoja na Raheem Sterling kama Mafowadi wake.

Uso kwa Uso
-England na Russia zimekutana mara 2 tangu Russia izaliwe upya kutoka Soviet Union na mar azote ilikuwa kwenye Mechi za kufuzu Fainali za EURO 2008 ambako England ilishinda 3-0 Uwanjani Wembley, London na Russia kushinda 2-1 huko Moscow.

-Wakiwa ndani ya Soviet Union, England iliifunga USSR 2-0 kwenye Mechi ya kusaka Mshindi wa 3 wa Ubingwa wa Mataifa ya Ulaya Mwaka 1968 na USSR kuifunga England 3-1 kwenye Makundi ya EURO Mwaka 1988.