Wednesday, June 8, 2016

EVERTON YAMNASA MENEJA RONALD KOEMAN TOKA KWA SOUTHAMPTON

Everton wamekubaliana na Klabu wenzao wa Ligi Kuu England Southampton ili kufungua njia Meneja wa Klabu hiyo maarufu kama ‘Watakatifu’ Ronald Koeman kuhamia kwao.
Everton watapaswa kuilipa Southampton fidia ya Pauni Milioni 5 ili Koeman, Raia wa Holland mwenye Miaka 53, kuwa Meneja wao mpya baada ya kudumu huko kwa Miaka Miwili.

Kwa sasa Everton haina Meneja baada ya kumtimua Roberto Martinez mwishoni mwa Msimu uliomalizika Mwezi uliopita.
Inatarajiwa Koeman atathibitishwa rasmi ifikapo Ijumaa na akiwa huko Everton ataambatana na Ndugue Erwin na Kocha wa Viungo Jan Kluitenberg.

Chini ya himaya ya Koeman, Southampton ilifanya vyema katika Historia yao kwa kumudu Nafasi za 7 na za 6 kwenye Ligi Kuu England katika Misimu Miwili iliyopita.

Koeman, ambae amewahi kuziongoza Klabu za Vitesse Arnhem, Ajax, Benfica, PSV, Valencia, AZ Alkmaar, Feyenoord na hii Southampton, amewahi kutwaa Ubingwa wa Holland akiwa na Klabu za Ajax na PSV.
Akiwa Mchezaji, Koeman alicheza Mechi 763 na kufunga Mabao 253 huku akitwaa Ubingwa wa Ulaya akiwa na Holland Mwaka 1988.
Pia ameshatwaa Klabu Bingwa Ulaya Mwaka 1988 akiwa na PSV Eindhoven na Mwaka 1992 akiwa na Barcelona huku yeye akifunga Bao la ushindi dhidi ya Sampdoria Uwanjani Wembley.