Tuesday, June 21, 2016

HENRIKH MKHITARYAN AJISOGEZA KWA KARIBU NA KLABU YA MANCHESTER UNITED

KIUNGO wa Borussia Dortmund Henrikh Mkhitaryan anataka kuhamia Manchester United ili ajiunge na Klabu ya ‘ndoto zake’ kwa mujibu wa Wakala wake.
Mkhitaryan, mwenye Miaka 27, amekuwa akihusishwa sana na kuihama Dortmund katika kipindi hiki hasa kwa vile Mkataba wake umebakiza Mwaka Mmoja na mazungumzo ya kuuongeza yamevunjika.
Wakala wa Mchezaji huyo, Mino Raiola, amedai Man United ilishatoa Ofa ya Euro Milioni 24 kumnunua na kukataliwa na Dortmund huku Arsenal pia wakimvizia.

Hata hivyo, Dortmund imeng’ang’ania haina mpango wa kumuuza na watambakiza Mkhitaryan hata kama ataondoka bure mwishoni mwa Msimu huu mpya unaokuja.

Akiongea na Gazeti la Bild la huko Germany, Raiola ameeleza: “Tunaelewana na Mkuu wa Dortmund Hans-Joachim Watzke lakini sasa hatabiriki mara yuko hivi, mara anageuka lakini tunatarajia tutaafikiana tu!”

Raiola ameongeza: “Ofa kutoka Manchester United inakuja mara moja tu katika maisha ya Mchezaji na hakuna anaejua kama Msimu ujao milango itakuwa wazi kwa Micki! Manchester ndio Klabu ya ndoto za Micki na anataka kujiunga nao kwa njia yeyote ile!”

Alipobanwa zaidi na Bild kwamba inapaswa Man United waongeze Dau zaidi ya Euro Milioni 24 ili wamchukue Mkhitaryan, Raiola alisema: “Hiyo si kazi yangu. Kazi yangu ni kuwakilisha maslahi ya Mchezaji. Inajulikana nini Micki anataka!”