Monday, June 27, 2016

FULL TIME: ITALY 2 v 0 SPAIN, GIORGIO CHIELLINI NA PELLE WAIFUMUA SPAIN NA KUWATOA NJE!

NDANI ya Uwanja wa Stade de France Mjini Paris Nchini France, Mabingwa Watetezi Spain Leo wamevuliwa Taji lao baada ya kuchapwa 2-0 na Italy katika Mechi ya Raundi ya Mtoano ya Timu 16.
Italy walifunga Bao lao la Kwanza Dakika ya 33 baada ya Eder kupiga Frikiki ambayo iliokolewa na Kipa De Gea na kumkuta Giaccherini alieucheza Mpira na De Gea kuupiga tena kwa Mguu wakati akiwa amelala chini lakini ukamkuta Giorgio Chiellini alieutumbukiza wavuni.
Bao hilo lilidumu hadi Haftaimu.
Kipindi cha Pili Spain walikuja juu lakini walishindwa kuipenya ngome ngumu ya Italy ikongozwa na Chiellini na Bonucci.

Lakini Italy nao walikuwa hatari mno kwa kaunta-ataki ambazo mara kadhaa Spain waliokolewa na umahiri wa Kipa wao David De Gea.
Giorgio Chiellini akishangilia baada ya kuziona nyavu za Spain Usiku huu, Bao la pili limefungwa na Pelle dakika za lala salama.
Hata hivyo, katika Dakika ya 92, pasi ndefu ya Insigne toka Winga ya Kushoto kwenda Winga ya Kulia ilimkuta Darmian ambae Krosi yake ilimbabatiza Sergio Ramos na kumfikia Graziano Pelle ambae alikuwa uso kwa uso na Kipa De Gea na hakufanya kosa kukwamisha Mpira wavuni na kuipa Italy Bao lao la Pili.

Sasa Italy wametinga Robo Fainali ambapo watacheza na Germany hapo Jumamosi.
Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya EURO 2016 itamalizika Leo Usiku huko Mjini Nice kwa Mechi kati ya England na Iceland.