Tuesday, June 14, 2016

JUVE YAMSAINI KIUNGO WA AS ROMA MIRALEM PJANIC!

MABINGWA wa Italy Juventus wamemsaini Miralem Pjanic kutoka kwa Wapinzani wao wa Serie A AS Roma.
Kiungo huyo wa Bosnia-Herzegovina mwenye Miaka 26 amenunuliwa kwa Dau la Pauni Milioni 25.4 na kusaini Mkataba wa Miaka Mitano.
Pjanic, ambae alifuzu upimwaji wa Afya yake hii Leo, alijiunga na AS Roma Mwaka 2011 akitokea Klabu ya France Lyon.

Msimu huu uliokwisha Mei, Pjanic alifunga Bao 10 na kutengeneza 12 katika Mechi zake 33 za Serie A akiisaidia AS Roma kumaliza Nafasi ya 3 ikiwa Pointi 11 nyuma yay a Mabingwa Juve.

Katika Maisha yake ya Soka, Pjanic alianzia huko Metz ya France Mwaka 2007 kuichezea Timu ya Kwanza na 2008 kujiunga na Lyon ambako alikaa hadi 2011 na kujiunga na AS Roma.

Akiwa na AS Roma, Pjanic alicheza Mechi 159 na kufunga Bao 27.

Pia, Kiungo huyo, ambae alianzia kuchezea Timu za Vijana za Luxembourg, alichezea Timu ya Kwanza ya Taifa la Bosnia-Herzegovina kuanzia 2008 na kucheza Mechi 68 akifunga Bao 11.

Inaaminika Juve wameamua kumchukua Miralem Pjanic kuwa mbadala wa Kiungo wao Paul Pogba ambae zipo habari nzito atahama huku akidaiwa kugombewa na Real Madrid na Klabu yake ya zamani Manchester United.