Monday, June 27, 2016

KUSTAAFU LIONEL MESSI ARGENTINA, AGUERO ADAI WENGI ZAIDI KUNG’ATUKA AKIWEMO YEYE!

Sergio Aguero amedai wapo Wachezaji wengi zaidi wanao tafakari kumfuata Lionel Messi na kutangaza kustaafu kuichezea Nchi hiyo huku na yeye mwenyewe akiwa miongoni mwao.
Argentina Alfajiri ya Jumatatu walipokea kipigo chao cha tatu cha Fainali kubwa katika Miaka Mitatu baada ya kubwagwa kwa Penati 4-2 na Chile kwenye Fainali ya Copa America Centenario iliyochezwa USA.
Mwaka Jana Argentina walibwagwa kwa Penati na Chile huko Santiago, Chile kwenye Fainali ya Copa America na Mwaka Juzi walifungwa 1-0 na Germany kwenye Fainali ya Kombe la Dunia huko Brazil.

Akiongea baada ya Messi kutangaza kustaafu kuichezea Argentina, Aguero alisema: “Pengine Messi hatakuwa peke yake kuondoka Timu ya Taifa. Wapo Wachezaji kadhaa wanaotafakari kubaki au kuondoka!”

Alipohojiwa kuhusu kustaafu kwa Messi, Aguero, mwenye Miaka 28, alisema hajawahi kumuona mwenzake huyo, ambae amecheza Soka nae tokea utotoni, akiwa amevunjika moyo kabisa.

Aguero alieleza: “Kwa bahati mbaya, Mtu pekee alievunjika moyo kiasi kikubwa ni yeye. Sijawahi kumuona hali ile. Alijaribu kila awezalo kutufikisha hapa!”

Messi amestaafu baada ya kuichezea Argentina mara 113 wakati Aguero amecheza mara 76.