Monday, June 27, 2016

LIVERPOOL, SOUTHAMPTON ZAAFIKI, SADIO MANE APIMWA AFYA ANFIELD!

STRAIKA wa Southampton Sadio Mane atapimwa afya yake hii Leo baada ya Southampton kukubali Dau la Liverpool la Pauni Milioni 30 kumnunua.
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amevutiwa sana na Mchezaji huyu wa Kimataifa kutoka Senegal ambae aliiua Liverpool Machi 20 kwa kufunga Bao 2 wakati Southampton ikitoka nyuma 2-0 na kuifunga Liverpool 3-2 huko Saint Mary Stadium.
Dili hii inaingia miongoni mwa Dili kali za Liverpool pamoja na zile za kulipa Pauni Milioni 32.5 kumnunua Christian Benteke na ile ya Pauni Milioni 35 kumnunua Andy Carroll.
Msimu uliopita, Mane, ambae alihamia Southamton kutoka Salzburg kwa Pauni Milioni 10 Miaka Miwili iliyopita, aliifungia Southampton Bao 11 za Ligi Kuu England katika Mechi zake 37.

Ujio wa Mane utaongeza nguvu Fowadi ya Liverpool ambao Mafowadi wao wengine ni Daniel Sturridge, Divock Origin na Christian Benteke.
Mane anafuata mlolongo wa Wachezaji kadhaa wa Southampton kuhamia Liverpool ambapo tangu 2014, Adam Lallana, Dejan Lovren, Rickie Lambert na Nathaniel Clyne wote walitua Anfield.

Katika Kipindi hiki, Mane anakuwa Mchezaji wa Pili kuuzwa na Southampton, ambayo haina Meneja baada ya Ronald Koeman kuhamia Everton hivi Juzi, baada ya Mkenya Victor Wanyama kuhamia Tottenham kwa Dau la Pauni Milioni 11.