Tuesday, June 28, 2016

LIVERPOOL WAMSAINI SADIO MANE LEO, AWEKA REKODI YA MCHEZAJI WA BEI GHALI TOKA AFRIKA KATIKA HISTORIA!

Liverpool wamekamilisha kumsaini Sadio Mane kwa Dau la Pauni Milioni 34 kutoka Southampton na kumpa Mkataba wa Miaka Mitano.
Dau hilo linaweza kupanda na kufikia Pauni Milioni 36 likizidi lile la Mchezaji alienunuliwa na Liverpool kwa ghali kupita yeyote walipotoa Pauni Milioni 35 kumnunua Andy Carroll Mwaka 2011.
Dili hii imemfanya Mane, anaetoka Senegal, kuwa ndie Mchezaji wa Bei ghali kupita yeyote katika Historia akilipiku lile la Januari 2015 ambalo Man City walilipa Pauni Milioni 28 kwa Swansea City kumnunua Wilfried Bony.

Mane, ambae alifunga Bao 21 katika Gemu 67 za Ligi Kuu England alizochezea Southampton tangu ahamia hapo kutoka Salzburg Mwaka 2014, anakuwa Mchezaji wa Tatu kusainiwa na Meneja Jurgen Klopp katika kipindi kufuatia Kipa wa Germany Loris Karius na Beki wa Cameroon Joel Matip. Mane anafuata mlolongo wa Wachezaji kadhaa wa Southampton walionunuliwa na Liverpool tangu 2014 na wengine ni Adam Lallana, Dejan Lovren, Rickie Lambert na Nathaniel Clyne.