Wednesday, June 22, 2016

MAN UNITED YAONGEZA DAU KUMNASA MKHITARYAN TOKA DORTMUND

Baada ya Ofa yao ya kwanza kukataliwa na Borussia Dortmund, ripoti zimetoboa kuwa Manchester United, chini ya Meneja Mpya Jose Mourinho, imeongeza Dau lao hadi Pauni Milioni 28 ili kumnasa Henrikh Mkhitaryan.
Baada ya kumnunua Beki Eric Bailly hivi karibuni na pia kumchukua Supastaa wa Sweden Zlatan Ibrahimovic muda wowote kuanzia sasa, Mourinho ana matumaini makubwa kumpata Mkhitaryan.
Inasemekana Dortmund wanamthamini Mkhitaryan, mwenye Miaka 27 na ni Mchezaji wa Kimataifa wa Armenia, kwa Pauni Milioni 30 na wanatia ngumu kumuachia Mchezaji huyo ambae amebakisha Miezi 12 tu kwenye Mkataba wake na Mwakani anaweza kuondoka bure.

Dortmund wanatia ngumu hasa baada ya kuwapoteza Wachezaji Wawili katika kipindi hiki ambao ni Ilkay Gundogan aliehamia Man City na Mats Hummels alieenda Bayern Munich.
Lakini nao Dortmund pia wapo kwenye wakati mgumu kwani Mkhitaryan, aliewafungia Bao 23 Msimu uliopita, amekataa Mkataba Mpya na kung’ang’ania kuondoka huku Wakala wake, Mino Raiola, akidai Man United ndio Klabu ya ‘ndoto zake’ Staa huyo.
Akiongea na Gazeti la Bild la huko Germany, Raiola ameeleza: “Tunaelewana na Mkuu wa Dortmund Hans-Joachim Watzke lakini sasa hatabiriki mara yuko hivi, mara anageuka lakini tunatarajia tutaafikiana tu!”

Raiola ameongeza: “Ofa kutoka Manchester United inakuja mara moja tu katika maisha ya Mchezaji na hakuna anaejua kama Msimu ujao milango itakuwa wazi kwa Micki! Manchester ndio Klabu ya ndoto za Micki na anataka kujiunga nao kwa njia yeyote ile!”

Alipobanwa zaidi na Bild kwamba inapaswa Man United waongeze Dau ili wamchukue Mkhitaryan, Raiola alisema: “Hiyo si kazi yangu. Kazi yangu ni kuwakilisha maslahi ya Mchezaji. Inajulikana nini Micki anataka!”