Tuesday, June 28, 2016

MENEJA HODGSON AJIUZULU, WACHAMBUZI WAMTUPIA MANENO! ROONEY NJE NDANI!

MENEJA wa England Roy Hodgson amejiuzulu kufuatia Jana kufungwa 2-1 na Iceland na kutupwa nje ya EURO 2016.
Hodgson, mwenye Miaka 68, amekuwa akiiongoza England kwa Miaka Minne sasa baada ya kumrithi Fabio Capello lakini ameshinda Mechi 3 tu kati ya 11 katika Fainali za Mashindano makubwa.
Mbali ya kutolewa kwenye EURO 2016, kule kupigwa na Iceland, Nchi ya Watu 330,000 tu na ambayo ndiyo iko chini kabisa kwenye Listi ya FIFA ya Ubora Duniani kwenye hizi EURO 2016 ikiwa Nafasi ya 34, ndiko kumeifedhehesha England.

Akitangaza kujiuzulu, Hodgson alisema: “Nasikitika tumemaliza namna hii lakini haya hutokea. Natumaini mtaiona Timu ya England kwenye Fainali kubwa hivi karibuni. Sasa ni wakati wa Mtu mwingine kuongoza kundi hili la Vijana wenye njaa na vipaji vikubwa mno.”

Hodgson, ambae alishinda Mechi 33 kati ya 56 alizosimamia England, alikuwa akimaliza Mkataba wake na England mara baada ya kumalizika Mashindano haya ya EURO 2016.

Chini ya usimamizi wa Hodgson, England ilitolewa kwa Penati na Italy kwenye Robo Fainali ya EURO 2014 na kushindwa kuvuka Makundi kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2014 huko Brazil.

England, ambao walifuzu Fainali za EURO 2016 wakishinda Mechi zao zote na kuwa ni Timu pekee kufanya hivyo, ilianza Fainali hizi kwenye Kundi B na kutoka Sare 1-1 na Russia, kuifunga Wales 2-1 na kisha kutoka 0-0 na Slovakia kwenye Mechi ambayo Hodgson alibadili Wachezaji 6 na kupondwa sana.

Hodgson pia alithibitisha kuwa Wasaidizi wake hapo England, Ray Lewington na Gary Neville, wataondoka.

Akiongea kuhusu uamuzi huo wa Hodgson, Mchezaji wa zamani wa England ambae sasa ni Mchambuzi wa BBC, Jermaine Jenas, alisema: “Jambo kubwa lililojitokeza ni kuwa Hodgson hakujua atendalo. Hakuijua Timu yake Bora wala Mfumo wake Bora. Ni njia mbaya kutupwa nje ya Mashindano!”

Nae Kepteni wa England ambae pia ni Kepteni wa Manchester United, Wayne Rooney, ameeleza: “Ni Siku ya huzuni kwetu. Siku zote kuna matokeo yasiyotegemewa kwenye Soka. Sio mbinu. Ni bahati mbaya. Tunajua sisi ni Timu nzuri. Siwezi kusimama hapa na kueleza hasa ni nini kimetokea. Mie nitabaki nikicheza. Tutaona nani mpya anakuja!”