Monday, June 27, 2016

MESSI ASTAAFU ARGENTINA

LIONEL MESSI ametangaza kustaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Argentina mara baada ya mapema Leo kupaisha Penati kwenye Mikwaju ya Penati Tano Tano wakati Argentina ikibwagwa kwa Penati 4-2 na Chile kwenye Fainali ya Copa America Centenario.
Akiongea baada ya Mechi hiyo Messi alisema: "Haya hayakupangwa kwangu. Kwangu mimi Timu ya Taifa imekwisha. Nimefanya kila niwezalo na inauma sana kutokuwa Bingwa."
Messi, mwenye Miaka 29, alianza kuichezea Argentina Mwaka 2005 na kucheza Mechi 115 ambapo Juzi alivunja Rekodi ya Ufungaji Bora Argentina ya Gabriel Batistuta kwa kupachika Bao 55.
Lakini ukiachia Medali ya Dhahabu ya Olimpiki aliyotwaa Mwaka 2008, Messi hajatwaa Taji lolote huku Argentina ikibwagwa katika Fainali kubwa 4.
Kuanzia 2014, Argentina na Lionel Messi, Mchezaji Bora Duniani mara 5, wamefika Fainali 3 na zote kufungwa.
2014 walicheza Fainali ya Kombe la Dunia huko Brazil na kufungwa na Germany 1-0 na Mwaka Jana kutolewa kwa Penati na Chile huko Santiago kwenye Copa America.

Leo Alfajiri huko USA, kwenye Fainali ya Copa America Centenario, Argentina na Chile zilitoka 0-0 katika Dakika 120 za Gemu na Gemu kuamuliwa kwa Mikwaju ya Penati.
Baada ya Chile kukosa Penati ya Kwanza, Messi akaja kuipigia Argentina Penati yao ya kwanza na kupaisha.
Argentina wakakosa Penati nyingine na Chile kushinda kwa Penati 4-2 na kubeba Kombe la Copa America Centenario.
Messi amekuwa na mafanikio makubwa na Timu yake ya Spain Barcelona ambayo ametwaa Ubingwa wa La Liga mara 8 na kubeba UEFA CHAMPIONZ LIGI mara 4.
Messi aliongeza: "Ni Fainali 4, nimejaribu. Ni kitu kikubwa nilichokitaka lakini sikupata sasa nadhani imekwisha. Ni bora kwa kila Mtu niondoke. Ni ngumu lakini uamuzi umefanyika. Sasa sitajaribu tena na sitabadili uamuzi."
Lakini Kipa wa Argentina ambae pia huchezea Manchester United, Sergio Romero, ana matumaini atatafakari uamuzi wake na kuubadili.
Amesema: "Nadhani aliongea wakati akiwa na munkari kwani tumeikosa nafasi kubwa. Nashindwa kuelewa Timu ya Taifa bila Messi itakuwaje!"