Saturday, June 25, 2016

MESUT OZIL NA PAUL POGBA WACHANGIA MATIBABU YA WATOTO 22 TANZANIA!

Mesut Ozil na Paul Pogba wamelipia matibabu ya Watoto 22 wa Tanzania ambao walihitaji kufanyiwa Operesheni.  Mchango huo wa Wachezaji hao wakubwa Duniani ambao kila mmoja alichangia kwa watoto 11 unapitia Kampeni ya Kundi la Hisani liitwalo BigShoe11 na matibabu hayo yalifanyika huko Ifunda Nchini Tanzania wakati huu wa Fainali za EURO 2016 chini ya Timu ya Madaktari wa Kimataifa.

Miaka Miwili iliyopita, Ozil, ambae ni Mchezaji wa Klabu ya Arsenal anaetoka Ujerumani, alisifiwa sana kwa kuchangia matibabu ya Watoto 23 wa Brazil wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zilizochezwa Nchini humo.

Jambo hilo lilimfanya Ozil atunukiwe Tuzo ya Laureus Sport for Good Mjini Berlin, Germany kwa ukarimu wake wa kutoa michango na kushiriki shughuli za hisani.

Hivi sasa Ozil yupo huko France akishiriki michuano ya EURO 2016 akiwa na Timu ya Taifa ya Germany.

Nae Paul Pogba, Mchezaji wa Juventus, pia yupo kwao France akichezea Nchi hiyo kwenye Fainali za EURO 2016.

Pogba na Ozil ni miongoni mwa Wachezaji wa kwanza kushirikishwa kwenye Kampeni ya BigShoe11 ya kusaidia matibabu ya Watoto na wao wenyewe wameahidi kila mmoja kusaka Wachezaji wengine 11 kila mmoja ambao ni vipenzi wao ili nao washiriki kutoa hisani kupitia Kampeni ya BigShoe11 kwa kuchangia matibabu ya Watoto 11 kila mmoja.