Sunday, June 19, 2016

MIRAJI ADAM: NIPO TAYARI KUICHEZEA TIMU YOYOTE YA LIGI KUU VPL.

BEKI wa Simba Miraji Adam ambaye alikuwa anachezea Coastal Union kwa mkopo amesema yupo tayari kucheza timu yoyote ligi kuu isipokuwa za daraja la kwanza.
Miraji ambaye mkataba wake na Simba unaelekea ukingoni ameamua kufunguka baada ya kuona viongozi wake wapo kimya wakati dirisha la usajili limeshafunguliwa. “Sijajua kama nitarejea Simba maana viongozi hawaeleweki na mkataba wangu na unaelekea ukingoni hivyo nipo tayari kuchezea timu yoyote isipokuwa ya ligi daraja la kwanza”, alisema Miraji
Pia Miraji amesema anaweza kuendelea kuichezea Simba endapo watafanya mazungumzo na kuelewana kwa sababu mpira ni kazi yake pia ana malengo kucheza mpira wa kulipwa siku za mbeleni.
Miraji anasema tatizo la kuandamwa na majeraha lilimuathiri ndiyo maana ailishindwa kucheza vizuri kwani alikuwa na uoga wa kuumia kila alipokuwa uwanjani, ila sasa anamshukuru Mungu yupo vizuri ndiyo maana aliweza kung’ara alipokuwa Coastal Union na kuzifunga Yanga na Azam FC katika michezo ya ligi kuu msimu uliopita.
Beki huyu wa pembeni ambaye ni mtaalamu wa kupiga mipira iliyokufa ameichezea Simba kwa miaka mitano akitokea timu ya vijana ya klabu hiyo ambayo imewahi kumtoa kwa mkopo katika timu za Mtibwa Sugar (2014/15 wakati wa mzunguko wa pili) na Coastal Union ya Tanga wakati wa mzunguko wa pili msimu uliopita.
Simba ilimchukua Miraji akitokea Azam FC B kwani wakati huo Azam ilikuwa haina mpango wa kuchukua mchezaji kutoka kikosi cha pili kwenda kikosi cha kwanza hivyo aliona kuendelea kubaki aliona anajichelewesha kutimiza malengo yake.