Saturday, June 18, 2016

MKUU WA LEICESTER ADAI VARDY KUTOHAMIA ARSENAL!

MABINGWA wa Ligi Kuu England Leicester City wana matumaini Straika wao Jamie Vardy atakataa mpango wowote wa kumuhamisha kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wao Aiyawatt Srivaddhanaprabha.
Msimu uliopita Vardy aliifungia Leicester Bao 24 kwenye Ligi Kuu, akiwa Bao 1 nyuma ya Mfungaji Bora Harry Kane, na kuiwezesha Leicester kutwaa Ubingwa.
Hivi sasa Vardy yuko huko France akiichezea England kwenye EURO 2016 na Juzi alifunga Bao lao la kusawazisha wakati England ikitoka nyuma na kuifunga Wales 2-1 kwenye Mechi ya Kundi B la EURO 2016.

Vardy, mwenye Miaka 29, ameripotiwa kutaka kununuliwa na Arsenal kwa Dau la Pauni Milioni 20.
Vardy hivi Juzi alisema kuwa kwa sasa anatilia mkazo EURO 2016 lakini Srivaddhanaprabha ana Imani Mchezaji huyo atabaki Leicester.

Srivaddhanaprabha, ambae ni Mtoto wa Mmiliki wa Leicester Vichai Srivaddhanaprabha, amesema: “Mtaona habari hivi karibuni lakini atabaki.”
Leicester wataanza Msimu mpya wa 2016/17 hapo Agosti 7 kwa kucheza Wembley Jijini London na Mabingwa wa FA CUP Manchester United katika Mechi ya kufungua pazia Msimu mpya ya kugombea Ngao ya Hisani na hapo Agosti 13 wataanza utetezi wa Taji lao la Ligi Kuu England Ugenini na Hull City iliyopanda Daraja.