Saturday, June 25, 2016

REAL MADRID NA BARCA WAMTUPIA JICHO JESUS!

Wapinzani wa Jadi huko Spain, FC Barcelona, na Real Madrid, wamejitumbukiza kwenye mvutano wa kumgombea Kinda wa Brazil anaechezea Klabu ya huko, Palmeiras, aitwae Gabriel Jesus.
Mbali ya Vigogo hao wa Spain kumgombea, Kinda huyo wa Miaka 19, pia anawaniwa na Klabu nyingine kubwa za Ulaya zikiwemo Juventus na Bayern Munich.

Msimu huu, Jesus ameifungia Palmeiras Bao 6 katika Mechi zake 10 na Dau lake la kumnunua linakadiriwa kuwa Euro Milioni 24.

Mwaka Jana, Jesus aliteuliwa kuwa ndie Mchezaji Mpya Bora wa Campeonato Brasileiro Série A baada ya kuisaidia Palmeiras kutwaa Copa do Brasil.

Lakini, kama ilivyo kwa Wachezaji wengi wa Brazil, kumnunua Jesus ni Biashara yenye utata sana kwani umiliki wake kibiashara unahusu pande nyingi.

Kibiashara, Jesus anamilikiwa na pande 3 ambazo ni Mchezaji mwenyewe, Wawakilishi wake na Klabu ya Palmeiras.