Saturday, June 11, 2016

UCHAGUZI YANGA: DRFA YATAKA HERI, JANA MAHAKAMA YATUPA NJE PINGAMIZI!

WAKATI DRFA ikiwataka Wanayanga kufanya Uchaguzi Mkuu wao kwa utulivu, Mahakama ya Haklimu Mkazi ya Kisutu Jana ilitupa nje pingamizi la Uchaguzi huo lililopelekwa huko Dakika za mwishoni.
Mwenyekiti wa DRFA, Chama cha Soka cha Dar es Salaam, Almas Kasongo, amewataka Wanachama wa Yanga kufanya Uchaguzi Mkuu wao kwa amani na utulivu.

Kasongo ameomba utulivu kwa Klabu hiyo kubwa ambayo Msimu huu wametetea vyema Taji lao la Ubingwa wa Ligi Kuu Vodacom na pia kubeba Kombe la Shirikisho, maarfufu kama Azam Sports Federation Cup na pia kuwa Klabu pekee Nchini Tanzania kuendelea kuwepo kwenye Mashindano ya Kimataifa.

Yanga wametinga Hatua ya Makundi ya Mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikishona wapo Kundi A pamoja na Vigogo TP Mazembe ya Congo DR, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Kwenye Mashindano hayo, Yanga wataanza Ugenini huko Algeria na MO Bejaia hapo Jumatatu Juni 20.

WAKATI HUO HUO, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam, Huruma Shaidi, Jana alitupilia mbali pingamizi lililoletwa na Wanachama Watatu wa Yanga, Kingamba Kingwamba, Juma Matimbwa and Siwema Chokota, kusimamisha Uchaguzi Mkuu wa Yanga unaotarajiwa kufanyika Leo huko Diamond Jubelee Hall Jijini Dar es Salaam.

Hakimu Huruma Shaidi ameripotiwa kusema: “Tutafute haki na si vitu vya ujanja. Ninachoona, maombi haya yameletwa Dakika ya mwisho yakiwa na lengo baya.”

“Michezo ni starehe ya Watu wengi. Tufanye vitu vya kuendeleza michezo na si kuhujumu. Kwa sababu hiyo, natupilia mbali maombi haya.”

Imeripotiwa kuwa Mwanasheria wa Wanachama hao Watatu Walioleta pingamizi, Julius Manjeka, akiwasilisha Hati ya Dharura kuusimamisha Uchaguzi huo aliiambia Mahakama kuwa ipo Amri ya Mahakama ya Julai 1, 2010 inayotaka Yanga kuteua Kamati Maalum ya kuedesha Mikutano, Uchaguzi na shughuli za Yanga za Wadhamini wake na hivyo kufanyika kwa Uchaguzi wa Leo ni kupinga Amri hiyo.

Lakini Hakimu Huruma Shaidi, akipinga hilo alitaja kuwa Amri hiyo ilitolewa tangu 2010 na kusema: “Ikiwa tangu wakati huo hakuna kilichofanyika, basi wale waliobebeshwa Amri hiyo walilalia haki yao. Kama walipaswa kufanya kitu basi ni kuleta maombi ya kutimizwa Amri hiyo na si maombi haya.”

Kwenye Uchaguzi wa Leo, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, na Makamu wake, Clement Sanga, ndio Wagombea pekee wa Nafasi hizo huku pia wapo Wanachama kadhaa wanaowania Nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Yanga.