Saturday, June 25, 2016

VARDY ANENA KWANINI ALIIKATAA ARSENAL, WENGER AHESHIMU UAMUZI WAKE!

WAKATI Jamie Vardy akipasua kwanini alikataa kujiunga na Arsenal, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema anaheshimu uamuzi wa Straika huyo kuamua kubali Leicester City.
Jana Leicester ilitangaza uthibitisho wa Vardy kubakia kwao ambako amepewa Mkataba mpya wa Miaka Minne.

Leo Vardy ametoboa kuwa sababu kubwa iliyomfanya asiikubali Arsenal ni staili yao ya uchezaji ambayo haiendani na uchezaji wake.
Arsenal hutumia mtindo wa kumiliki mpira na pasi nyingi wakati Vardy amezoea staili ya Meneja wao Claudio Ranieri ya kaunta-ataki na kuchomoka kwa kasi kwenda kulisakama Goli la Wapinzani.
Pia Vardy anaamini Leicester wana Kikosi spesho kilichoshikamana na wanao uwezo kutetea Taji lao la Ubingwa wa England na vile vile kuleta mtikisiko kwenye UEFA CHAMPIONS LIGI.

Lingine ni kuwa Vardy, mwenye Miaka 29, alikosa kuhakikishiwa na Wenger kuwa hatatumiwa kwenye pozisheni nyingine kama vile Arsenal wafanyavyo kuwatupa Mastraika kwenye Winga.

Kutoka huko Emirates, Wenger Leo hii ametamka kuwa anauheshimu uamuzi wa Vardy kuamua kubaki na Leicester na kumtakia kila la heri.

Wenger ameeleza: “Tulimfuatilia na kumtaka. Sasa ameamua kubaki Leicester na tunamtakia heri. Yeye amechomoza kwenye Gemu akiwa mkubwa na Leicester wanastahili kwani ndio wamemwibua toka Timu ndogo Fleetwood mpaka akafanikiwa. Ana Miaka 29 na ameamua kubaki Leicester. Lazima uheshimu hilo!”