Tuesday, June 21, 2016

VICTOR WANYAMA NJIANI KUJIUNGA SPURS!

Tottenham Hotspur imeafikiana Dau la Pauni Milioni 11 na Southampton ili kumnunua Kiungo kutoka Kenya Victor Wanyama kwa mujibu wa duru za Soka toka huko Uingereza.
Inaaminika kuwa Wanyama, mwenye Miaka 24 na ambae alijiunga na ‘Watakatifu’ kwa Pauni Milioni 12.5 kutoka huko Celtic ya Scotland Julai 2013, ameshapimwa afya huko Spurs baada ya kuruka kutoka Kenya Jana.

Uhamisho huu utamfanya Wanyama kuungana tena huko Spurs na Meneja wake wa zamani Mauricio Pochettino ambae ndie alimchukua kutoka Celtic na kumpeleka Southampton.

Mwanzoni mwa Msimu uliopita, Wanyama aliomba kuondoka Southampton ili aende Spurs lakini akazuiwa na kubakia kwa ‘Watakatifu’ na kuwasaidia kumaliza Nafasi ya 6 kwenye Ligi Kuu England.
Tangu ajiunge na Southampton Julai 2013, Wanyama ameichezea Klabu hiyo Mechi 85 za Ligi na kufunga Bao 4.

Ikiwa Dili hii itakamilika, Wanyama atakuwa Mchezaji wa kwanza kusainiwa na Spurs kwa ajili ya Msimu mpya ambao pia watacheza UEFA CHAMPIONS LIGI kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.
Wanyama alisainiwa huko Celtic kutoka Klabu ya Belgium Germinal Beerschot Julai 2011 baada ya kwenda Ulaya kutoka Kenya Mwaka 2007 alipojiunga na Klabu ya Sweden Helsingborg.