Wednesday, June 22, 2016

ZLATAN IBRAHIMOVIC ANUKIA MANCHESTER UNITED MSIMU 2016-2017

MARA baada ya Jana Straika wa Sweden Zlatan Ibrahimovic kutangaza kustaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Nchi yake mara baada ya EURO 2016 kumalizika, zimeibuka habari kuwa tayari alishasaini kuichezea Manchester United.
Ripoti kutoka kwa Mwanahabari wa kuaminika kutoka Italy, Tancredi Palmeri, amedai Staa huyo ambae amemaliza Mkataba wake na Paris St-Germain, alisaini Makubaliano ya Kabla Mkataba mapema Juni akiwa Kambini na Sweden.
Mwezi wote huu, Ibrahimovic, mwenye Miaka 34, amekuwa akibanwa na Wanahabari kuhusu hatima yake na mwenyewe kuwajibu kwa utani mwingi.
Lakini, Palmeri, akiongea kwenye KKipindi cha TV cha Shoo ya Hawksbee and Jacobs, amesisitiza Makubaliano hayo ya kujiunga na Man United yalishainiwa na atajiunga Old Trafford kwa ajili ya Msimu ujao.
Mbali ya Man United, Ibrahimovic pia alikuwa akitajwa kwenda Klabu za Bayern Munich, AC Milan na Klabu kadhaa za MLS huko USA pamoja na za China.
Jana, akitangaza kustaafu kuichezea Sweden, Ibrahimovic alieleza: "Nasikia fahari kwa yote niliyofikia na Siku zote nitakuwa na Bendera ya Sweden!" 

Ibrahimovic ameifungia Sweden Mabao 62 na hiyo ni Rekodi ya Bao nyingi kwa Taifa hilo na akiichezea Sweden kwenye Mechi ya Jumatano na Belgium itakuwa ni Mechi yake ya 116 akiwa Mechi 32 nyuma ya Mshika Rekodi Anders Svensson aliechezea Mechi 148.
Sweden watatupwa nje ya EURO 2016 ikiwa watashindwa kuifunga Belgium Leo hii kwenye Mechi ya Kundi E itakayochezwa huko France lakini wakishinda watasonga Raundi ya Mtoano ya Timu 16.