Tuesday, July 26, 2016

ADA KUBWA YA WAKALA MINO RAIOLA KUZUIA POGBA KUTUA MAN UNITED!

UAMUZI wa nani ndie atabeba zigo la kulipa Ada kubwa ya Wakala wa Paul Pogba ndio umekwamisha Uhamisho wa Kiungo huyo kutoka Juventus kurudi tena Manchester United.

Baada ya mvutano wa Dau kamili la Uhamisho wa Pogba kufikia makubaliano kati ya Juve na Man United huku pia Maslahi binafsi ya Mchezaji huyo kuridhiwa, sasa ripoti zinadai Ada kubwa ya Wakala wa Pogba, Mino Raiola, Mzaliwa wa Holland mwenye asili ya Italy ndio kikwazo kikubwa.

Inaaminika Juve na Man United zimeafikiana kulipwa zaidi ya Euro Milioni 100 kama Ada ya Uhamisho huku Mchezaji huyo akilipwa Euro Milioni 13 kwa Mwaka kama Mshahara wake lakini pia Wakala anatakiwa kulipwa Asilimia 20 ya Malipo yote.

Kwa hilo, Minola anapaswa kulipwa Euro Milioni 24 kama Mgao wake lakini Juve inasisitiza ni Man United inapasa kulipwa Pesa hizo wakati Man United imekazania Fedha hizo zitokane na malipo yao na si ziada ya Malipo yao kwenye Ada ya Uhamisho.

Huku wakijua Man United sasa wamekataa kuburuzwa na huku pia wakitambua kwa Dau wanalotaka hakuna Klabu inayoweza kulipa, Juve wanahaha kuikamilisha Dili hii haraka iwezekanavyo kwa vile pia wakibanwa kwa sababu wanataka kumnunua Straika wa Argentina, Gonzalo Higuain, kwa Dau la Rekodi ya Italy kutoka Napoli.