Sunday, July 10, 2016

BARCELONA YAANZISHA KAMPENI #TodosSomosLeoMessi!

Lionel Messi anaesakamwa sana hivi sasa amepata sapoti kubwa toka Klabu yake ya Spain FC Barcelona ambayo imeanzisha Kampeni kubwa kwenye Mitandao ya Kijamii ili kumpa moyo.

Hivi karibuni Messi alistaafu kuichezea Timu ya Taifa ya Nchi yake Argentina baada ya kupoteza Fainali ya Copa America Centenario huko Marekani walipobwagwa kwa Mikwaju ya Penati na Chile ukiwa ni mlolongo wa Fainali za Mashindano makubwa Manne ya Mchezaji huyo kushindwa kutwaa Taji kubwa.

Na kabla kovu hilo halijapona, hapo Juzi Mahakama ya huko Spain ilimhukumu Kifungo cha Miezi 21 Jela na kuamriwa kulipa Faini ya Euro Milioni 2 baada ya kupatikana na hatia ya Ukwepaji Kodi.

Ili kukabili majanga hayo, Barcelona Leo imeanzisha Kampeni kwenye Mitandao ya Kijamii ikiwa na kiashiria #TodosSomosLeoMessi ikimaanisha ‘Sisi Sote ni Leo Messi’.
Barcelona imewaasa Mashabiki wao kuposti Picha zao wakiinua Vidole 10 ikiashiria Namba 10 ya Jezi ya Messi.

Taarifa rasmi ya Barcelona ilieleza: “Kampeni inawaasa Mashabiki wote wa Barca kuonyesha Imani yao kwa Mchezaji Bora Duniani kwa kumpa sapoti kwenye Mitandao ya Kijamii”

Nae Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu ametoa sapoti yake kwa kutoa posti ya Twitter "Leo, wale wanaokushambulia wewe wanaishambulia Barca na historia yake. Tutakulinda mpaka mwisho. Tuko pamoja daima!"

Messi, mwenye Miaka 29, ameisaidia Barcelona kubeba Ubingwa wa UEFA CHAMPIONS LIGI mara 4 na ule wa La Liga mara 8.