Saturday, July 2, 2016

MARIO BALOTELLI KURUDI ANFIELD

MCHEZAJI mtukutu Mario Balotelli atarudi Klabuni kwake Liverpool Jumamosi kuanza rasmi mazoezi kwa ajili ya Msimu mpya baada ya kukosa Klabu ya kumchukua.
Liverpool imewataka Wachezaji wao wote ambao hawakushiriki Fainali za EURO 2016 na COPA AMERICA kurejea Klabuni Jumamosi kuanza mazoezi chini ya Meneja wao Jurgen Klopp.

Balotelli, ambae alikuwa kwa Mkopo huko Nchini kwao Italy akiichezea AC Milan, nae yupo kwenye mkumbo huo na sasa anarejea Liverpool ambako katika Mechi zake 16 alizochezea alifunga Bao 1 tu.
Pamoja na Balotelli, Wachezaji Wanne Wapya wa Liverpool, Sadio Mane, Joel Matip, Marko Grujic na Kipa Loris Karius, wote wataripoti hiyo Jumamosi.

Tangu Februari, Liverpool iliamua kumtosa Balotelli ambako hata huko AC Milan alikokuwepo kwa Mkopo nyota ilififia na kufunga Bao 1 tu katika Mechi 20 kiasi cha kutemwa hata Kikosi cha Timu ya Taifa ya Italy.

Licha ya Liverpool kumfungulia milango, Wakala wa Balotelli, Mino Raiola, ameshindwa kumpatia Balotelli, mwenye Miaka 25, Klabu mpya ingawa Klabu za China na Uturuki zilionyesha nia.

Balotelli alianzia Soka lake kwenye Klabu ya Lumezzane na kucheza Mechi 2 na mara mbili alifanya majaribio na Barcelona na kushindwa.

Mwaka 2007, Balotelli akajiunga na Inter Milan ambako Kocha Roberto Mancini akamchezesha Timu ya Kwanza lakini baada ya Mancini kuondoka utukutu wa Balotelli ukapindukia na akawa na uhusiano mbovu na Meneja Mpya Jose Mourinho ambae alimsimamisha kuchezea Timu ya Kwanza.

Roberto Mancini, akiwa Manchester City, aliamua kumchukua Balotelli na Agosti 2010 akajiunga nae hapo City lakini wakakwaruzana Januari 2013 na Mchezaji huyo akauzwa kwa AC Milan alipokaa Miezi 18 na kununuliwa na Liverpool kwa ajili ya Msimu wa 2014/15 ambao haukuwa na mafanikio kwake na kisha kupelekwa kwa Mkopo AC Milan.

Balotelli ameichezea Timu ya Taifa ya Italy mara 30 na kuiwakilisha Nchi hiyo kwenye Mashindano ya UEFA Euro 2012, 2013 FIFA Kombe la Mabara na 2014 FIFA Kombe la Dunia.