Monday, July 25, 2016

MECHI YA MANCHESTER UNITED V MANCHESTER CITY 'YAPIGWA STOP LEO'

DABI ya Klabu za Manchester iliyokuwa ichezwe Leo huko Beijing, China kati ya Manchester United na Manchester City imefutwa.

Uthibitisho wa kufutwa Mechi hii ulitolewa pia kwenye Tovuti ya Klabu ya Man United iliyotoa taarifa fupi ikisema kuwa sababu za Hali ya Hewa mbaya iliyoikumba Mji wa Beijing ambapo kumekuwa na Mvua kubwa kumewafanya Waandaaji wa Mechi na Klabu zote mbili ziafiki kufutwa kwa Mechi hii.

Uwanja wa kuchezea wa Bird's Nest Stadium umeharibika kiasi kuufanya usiweze kuchezewa Mechi na kuhatarisha usalama wa Wachezaji.
Jana Meneja wa Man United, Jose Mourinho, alibainisha kuwa Uwanja huo upo kwenye hali mbaya.

Nae Meneja wa City, Pep Guardiola, nae alikuwa na msimamo huo huo na kutoa hofu yake kuhusu kuumia kwa Wachezaji kwenye hali hiyo ya Uwanja.

Klabu zote mbili zilishindwa kuutumia Uwanja wa Bird's Nest kwa ajili ya Mazoezi yao ya mwisho na kulazimika kutumia Uwanja mwingine.

Jana Mvua iliendelea kunyesha huko Beijing na Leo pia Mvua zaidi imetabiriwa.

Juzi, Ndege moja kati ya mbili zilizowabeba Kikosi cha Man United, ilishindwa kutua Uwanja wa Ndege wa Beijing kutokana na Radi na Mvua kubwa na kulazimika kwenda kutua kwa dharura huko Tianjin, Kilomita 160 kutoka Beijing.