Thursday, July 28, 2016

PEP GUARDIOLA: WACHEZAJI WA CITY 'MATIMBWA' MARUFUKU MAZOEZINI!

 MENEJA wa Manchester City Pep Guardiola amepiga marufuku utumiaji wa Vyakula vya ovyo na pia kuzuia Wachezaji waliozidi uzito kufanya Mazoezi na Kikosi cha Kwanza.
Amri hizo zimedokezwa na Beki wa City Gael Clichy ambae amesema Wachezaji wamekatazwa kula vyakula kama Pizza, juisi za aina kadhaa na baadhi ya 'vyakula vizito'.
Clichy ameeleza: "Kwangu mie, hii ni mara ya kwanza Meneja amefanya kitu namna hii. Wapo Wachezaji kadhaa sasa hawafanyi mazoezi na Timu."
Aliongeza: "Ukiwa una uzito wa ziada hufanyi mazoezi na Timu. Lazima ujue kama una Kilo 60 na sasa una Kilo 70 huwezi kucheza Soka!"
City sasa wako kwenye Mazoezi ya kujitayarisha na Msimu mpya na Alhamisi watacheza Mechi ya International Champions Cup huko Shenzen, China na Borussia Dortmund.
City watanza Msimu wao mpya wa Ligi Kuu England kwa kucheza kwao Etihad na Sunderland hapo Agosti 13.