Thursday, July 28, 2016

PSG YAITWANGA 3-1 REAL MADRID, BAYERN YABWAGWA NA AC MILAN KWA PENATI 5-3

MFULULIZO wa Mechi za Kirafiki za kujipima kabla Msimu mpya kuanza chini ya mwamvuli wa Mashindano ya International Champions Cup umeendelea hapo Jana.
Huko Ohio, mbele ya Mashabiki.86,000, Paris Saint-Germain iliichapa Real Madrid Bao 3-1 wakati huko Soldier, Chicago, Illinois, Bayern Munich na AC Milan zilitoka 3-3 na Milan kuibuka kidedea kwa Penati 5-3.
Chini ya Kocha wao mpya Unal Emery, PSG sasa wamefanikiwa kushinda Mechi zao zote 3 za kujipima.
Hapo Jana Bao za Kipindi cha Kwanza za Thomas Meunier, Bao 2, na Nanitamo Ikone ziliibwaga Real iliyowakosa Mastaa wao wengi.
Bao pekee la Real katika kipigo hicho cha 3-1 lilifungwa kwa Penati ya Marcelo ya Dakika ya 44.
Kwenye Mechi hii, Real iliwakosa Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Luka Modric, James Rodriguez na Pepe huku Kocha Zinedine Zidane akiwachezesha Chipukizi na kuwaingiza 11 katika Kipindi cha Pili akiwemo Mwanawe Enzo.
Tofauti na Real, PSG walishusha Kikosi imara kikiongozwa na Nahodha Thiago Silva aliedumu Dakika 11 tu na kutolewa baada kuumia Paja.
Nao Bayern Munich na AC Milan zilitoka Sare ya Bao 3-3 katika Dakika 90 na Mshindi kuibuka AC Milan kwa Penati 5-3.
Bao za Bayern zilifungwa na Frank Ribery, Bao 2, na David Alaba wakati za AC Milan zilipachikwa na Niang, Bertolacci na Kucka.