Saturday, July 2, 2016

RYAN GIGGS AONDOKA OLD TRAFFORD

RYAN GIGGS na Manchester United Leo wamepeana mkno wa kwa heri baada ya Lejendari huyo kuamua rasmi kuondoka Klabuni hapo baada ya kukaa Miaka 29.
Leo Giggs, mwenye Miaka 41 na ambae alikuwa amebakisha Mwaka Mmoja kwenye Mkataba wake wa sasa, alitoa rasmi barua ya kushkuru na pia kuwaaga rasmi Mashabiki wa Man United huku nae Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Klabu hiyo, Ed Woodward, akimuaga na kutoa shukrani zake kwake.

Mara baada ya kuteuliwa Meneja Mpya Jose Mourinho, Giggs, ambae wadhifa wake ni Meneja Msaidizi, alipewa nafasi nyingine Klabuni lakini Mchezaji huyo, ambae aliichezea Man United Mechi 963, hakuafikiana na Klabu kuhusu hilo na sasa anasaka nafasi nyingine kujikita kama Meneja kitu ambacho anaruhusiwa kwa vile anayo UEFA Pro Licence inayomruhusu kufundisha Klabu ya Ligi Kuu England.

Giggs, aliezaliwa Mjini Cardiff huko Wales, alijiunga na Man United akiwa na Miaka 14 na akawa Profeshenali kamili Novemba 1990 akiwa na Miaka 17 na kucheza Mechi ya Kwanza ya Timu ya Kwanza dhidi ya Everton hapo Machi 2, 1991.

Akiaga, Giggs amesema: “Baada ya Miasimu 29 na Manchester United kama Mchezaji na Meneja Msaidizi, najua ushindi upo kwenye vinasaba vya Klabu hii, kutoa nafasi kwa Vijana na kucheza soka la kushambulia na kuvutia. Ni afya njema kuwa na matumaini makubwa, ni sawa kutegemea ushindi. Manchester United inategemea, inastahili, ushindi na si kinginecho.”

“Na ndio maana ni uamuzi mkuwa kwangu mimi kuondoka Klabu ambayo imekuwa ni maisha yangu tangu nina Miaka 14. Ni uamuzi ambao sikuuchukua kirahisi. Ninaondoka na kumbukumbu nyingi spesho na pia uzoefu wa maisha yote, ambao natumai utanisaidia maishani. Sasa ni wakati muafaka ingawa sina mipango ya kuingia Umeneja wa Soka kwa haraka lakini ndicho ninachokitaka.”

Nae Ed Woodward aliongea: “Sehemu ya Ryan kwenye Historia ya Manchester United ina uhakika…….Kila Mtu kwenye Klabu hii anamtakia heri na mafanikio katika maisha yake mapya. Tutamkosa lakini daima anakaribishwa Manchester United.”

Akiwa na Man United, Giggs alitwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13, UEFA CHAMPIONZ LIGI mara 2, FA CUP 4 na Kombe la Ligi mara 4 na kuweka Rekodi kuwa ndie Mchezaji pekee alietwaa Mataji mengi kiasi hicho huko Uingereza.

Giggs aliiongoza Man United kama Kaimu Meneja 2013 alipofukuzwa David Moyes na kusimamia Mechi 4 za mwisho za Ligi na kisha kuteuliwa Meneja Msaidizi Mwaka 2014 Louis van Gaal alipoteuliwa Meneja.