Saturday, July 2, 2016

RYAN GIGGS -KUNG’OKA MANCHESTER UNITED BAADA YA MIAKA 29!

RIPOTI zimeibuka kuwa Ryan Giggs ataondoka Manchester United baada ya kukubaliana na uongozi.
Man United inatarajiwa kutoa Taarifa rasmi hapo baadae.
Giggs, mwenye Miaka 42, amebakisha Mwaka Mmoja kwenye Mkataba wake wa sasa na ataondoka baada ya kuitumikia Klabu hiyo kwa Miaka 29.

Giggs, ambae wadhifa wake ni Meneja Msaidizi, alipewa nafasi nyingine Klabuni hapo baada ya kuchukuliwa Meneja Mpya Jose Mourinho ambae mwenyewe anataka Rafiki wake wa Siku nyingi, Rui Faria, ndie awe Meneja Msaidizi.
Inaelekea Giggs, ambae aliichezea Man United Mechi 963. hakuafikiana na Klabu kuhusu hilo na sasa anasaka nafasi nyingine kujikita kama Meneja kitu ambacho anaruhusiwa kwa vile anayo UEFA Pro Licence inayomruhusu kufundisha Klabu ya Ligi Kuu England.
Giggs, aliezaliwa Mjini Cardiff huko Wales, alijiunga na Man United akiwa na Miaka 14 na akawa Profeshenali kamili Novemba 1990 akiwa na Miaka 17 na kucheza Mechi ya Kwanza ya Timu ya Kwanza dhidi ya Everton hapo Machi 2, 1991.

Giggs ametwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13, UEFA CHAMPIONS LIGI mara 2, FA CUP 4 na Kombe la Ligi mara 4 na kuweka Rekodi kuwa ndie Mchezaji pekee alietwaa Mataji mengi kiasi hicho.
Giggs aliiongoza Man United kama Kaimu Meneja 2013 alipofukuzwa David Moyes na kusimamia Mechi 4 za mwisho za Ligi na kuteuliwa Meneja Msaidizi Mwaka 2014 Louis van Gaal alipoteuliwa Meneja.