Friday, July 1, 2016

SOUTHAMPTON YAMTEUA MFARANSA CLAUDE PUEL AWE MENEJA WAO MPYA!

Southampton imemteua Raia wa France Claude Puel kuwa Meneja wao mpya.
Puel, mwenye Miaka 54 na ambae aliwahi kuziongoza Klabu za Monaco na Nice huko France, amesaini mkataba wa Miaka Mitatu kumbadili Ronald Koeman aliehamia Everton hivi Juzi tu.
Puel atasaidiwa na aliekuwa Kocha wa Aston Villa, Erick Black, na pia Pascal Plancque na Dave Watson.
Puel ana kibarua kigumu cha kudumisha na kuendeleza mafanikio ya Koeman ambae kwenye Msimu uliopita ulioisha Mei alifanikiwa kuiweka Southampton Nafasi ya 6 kwenye Ligi Kuu England ambayo ndio nafasi ya juu kabisa Southampton kuwahi kuifikia.

Akiwa huko France, Puel alimudu kuipa Nice Nafasi ya 4 kwenye Ligi 1.
Puel, wakati akiwa Mchezaji, aliichezea Monaco zaidi Mechi 500 na kisha kuingia kwenye Umeneja wa Soka kuanzia 1999 na Mwaka 2000 aliiongoza Monaco kutwaa Ubingwa wa Ligi 1.

Baadae akahamia Lille na kudumu Misimu 6 na Mwaka 2008 akawa Lyon na baadae kwenda Nice alikokaa Miaka Minne.
Kazi kubwa ya kwanza itakayomkabili Mfaransa huyo ni kuziba mapengo ya Wachezaji waliohama ambao ni Sadio Mane aliekwenda Liverpool na Victor Wanyama ambae ameenda Tottenham.
Lakini tayari Southampton imeshamsaini Nathan Redmond kama mbadala wa Mane.