Saturday, July 16, 2016

TOKA TFF: STAND UNITED FC NI HALALI, TUZO 13 LIGI KUU YA VODACOM, UAMUZI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI.

STAND UNITED FC NI HALALI
Katika kikao chake cha 13 Julai 2016, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetoa msimamo kuhusu suala la Stand United kama ifuatavyo:-

Kamati imepitia vielelezo vyote na kujadiliana na wadau wa Stand United na kubaini bayana kwamba Stand United Football Club, ndiyo jina sahihi na halali lililosajiliwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo.

Uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye Klabu ya Stand United una sifa zote za kuitwa uchaguzi huru na wa haki kwa vile mchakato ulihusisha wanachama halali klabu hiyo.

Wanachama wa Stand United ambao hawakushiriki uchaguzi ikiwa ni pamoja na wale waliokwenda kundi la kampuni wana uhalali wa kuendelea kuwa wanachama wa Stand United.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa Stand United FC ni halali na ni ruksa kwao kuendesha ofisi na shughuli za Stand United kwa ujumla.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linatambua daftari la Wanachama wa Stand United lililoboreshwa kwa maelekezo ya TFF.


IMETOLEWA NA DOMINA MADELI –
MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA UCHAGUZI TFF WANAOWANIA TUZO 13 LIGI KUU YA VODACOM

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limetangaza wanamichezo wote wanaowania tuzo 13 kwenye hafla ya washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2015/2016 itakayofanyika Jumapili (Julai 17 mwaka huu) kwenye hoteli ya Double Tree by Hilton jijini Dar es Salaam.

Aina 13 za tuzo ya Ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania zitatolewa kwa washindi chini ya uratibu wa Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoundwa na waandishi wa habari za michezo, makocha, viongozi (administrators) na wawakilishi kutoka kwa wadhamini (Vodacom na Azam Tv).

uzo hizo na kiasi cha fedha wanazopata washindi kwenye mabano ni
Bingwa (sh. 81,345,723)
Makamu bingwa (sh. 40,672,861)
4. Mshindi wa nne (sh. 23,241,635)
5. Timu yenye Nidhamu Bora (sh. 17,228,820)

*Zilizopendekezwa kuwania tuzo hiyo ni:
- JKT Ruvu
- Mgambo Shooting na
- Mtibwa Sugar

6. Mchezaji Bora wa Ligi (sh. 9,228,820)
*Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo hiyo ni:
- Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar)
- Juma Abdul (Yanga) na
- Mohamed Hussein (Simba)
7. Mfungaji bora (sh. 5,742,940)
8. Kipa Bora (sh. 5,742,940)
 

Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo hiyo ni:
- Aishi Manula (Azam),
- Beno Kakolanya (Tanzania Prisons) na
- Deogratius Munishi (Yanga)

9. Mchezaji Bora wa Kigeni (sh. 5,742,940)
- Donald Ngoma (Yanga)
- Thabani Kamusoko (Yanga)
- Vincent Agban (Simba) 


10. Kocha Bora (sh. 8,000,000)
*Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo hiyo ni:
- Hans Van Pluijm (Yanga)
- Mecky Maxime (Mtibwa Sugar) na
- Salum Mayanga (Tanzania Prisons)

11. Mwamuzi bora (sh. 5,742,940)
*Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo hiyo ni:
- Anthony Kayombo
- Ngole Mwangole
- Rajab Mrope

12. Mchezaji Bora Chipukizi (sh. 4,000,000
*Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo hiyo ni:
- Farid Mussa (Azam)
- Mohamed Hussein (Simba)
- Mzamiru Yasin (Mtibwa Sugar) na
- Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar)
13. Goli bora la msimu (sh. 3,000,000)

*Kinyang'anyiro cha goli bora ni:
- Ibrahim Ajib (magoli mawili ) na
- Amisi Tambwe (goli moja)

UAMUZI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA HADHI ZA WACHEZAJI

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti, Richard Sinamtwa imebaini kasoro kwa Abajalo FC kumtumia mchezaji Laurent E. Mugia hivyo kuamua kumfungia mchezaji huyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa kanuni ya 36 (16) toleo la mwaka 2014 la Ligi Daraja la Pili kwa kosa la kuchezea klabu mbili katika msimu mmoja.

Kwa kuwa kanuni za Ligi Daraja la Pili mpaka Ligi Kuu zina upungufu unaofanyiwa mapitio pale kiongozi wa timu anapofanya udanganyifu wa usajili wa mchezaji bila kumshirikisha mchezaji, Kamati sasa imelazimika kutumia kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Ibara ya VII (10) ikinukuu:

“A team which will have committed a fraud on the identity of player or which will have allowed a suspended or non-qualified player to take part in match shall, lose the match and shall be completely eliminated from the competition as soon as the incriminating fact are clearly established by CAF organizing committee.” Mwisho wa kunukuu.

Kwa maelezo hayo, timu ya Abajalo FC inanyang’anywa pointi sita. Timu za Pamba SC na The Mighty Elephant wanapewa pointi tatu kila timu na magoli matatu.

Kamati inaagiza Sektretarieti kuwachukulia hatua na kuwapeleka katika vyombo vya Serikali viongozi wote wa timu ya Abajalo walioshiriki kubadilisha jina la mchezaji alilotumia akiwa na timu ya Kagera Sugar ili kufanikisha usajili wao na pia kwa kubadilisha tarehe, mwezi na mwaka wa kuzaliwa za mchezaji ili kufanikisha usajili wao kwa msingi kwamba waligushi

Uamuzi huu, ni wa mwisho na kwamba kama kuna ambaye hajaridhika, ana nafasi ya kukata rufaa kwenye CAS - Mahakama ya Mashauri ya Soka ya FIFA iliyoko Geneva, Uswisi.

Awali kwa nyakati tofauti, Pamba SC ya Mwanza na The Mighty Elephant ya Songea zilikata rufaa kuilalamikia Abajalo FC kwa kumtumia mchezaji wa Kaliua City ya Tabora, Laurence Mugia kutoka Kagera Sugar katika michezo ya mtoano wa Ligi Daraja la Pili kwa ajili ya kupanda daraja la kwanzaa huku wakijua kuwa ni kosa kwa mujibu wa kanuni.

MALINZI AWAPONGEZA KUULI, NDULANE
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Revocatus Kuuli na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi, Francis Ndulane.

Kuuli, Wakili msomi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF, ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga mkoani Tabora.

Kadhalika, katika uteuzi huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amemteua Ndulane ambaye ni Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro.

Katika salamu hizo, Rais Malinzi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa kuwateua viongozi hao wa TFF, akisema kwamba ameonyesha namna alivyo na imani na watendaji hao katika shughuli zao mbalimbali ikiwamo TFF.

WAAMUZI LIGI MBALIMBALI WAANZA KUJIPANGA

Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imeandaa kozi mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya kwa waamuzi katika michuano ya kimataifa sambamba na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa msimu wa 2016/2017.

Kozi hiyo MA (Members Associations) itaanza kwa waamuzi wenye Beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) ambao kwa sasa wako 18 hapa Tanzania na wengine 12 wa ‘Elite’ ikiwa na maana ya waamuzi wanaotarajiwa kuveshwa Beji za FIFA. Darasa la waamuzi hao litakuwa na waamuzi 30.

Waamuzi hao wenye Beji ya FIFA na wale wanaotarajiwa kuveshwa beji hiyo, wanatakiwa kuripoti Dar es Salaam Julai 23, 2016 ambako kwa mujibu wa ratiba wataanza program ya kozi hiyo kwa kupima kasi ya kukimbia siku inayofuata Julai 24, 2016 wakisimamiwa na wakufunzi kutoka FIFA.

Mara baada ya programu hiyo, kozi itaendelea kwa waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) na makamishna wa michezo kwa msimu wa 2016/2017 na kwamba wahusika wote watajigharamia gharama zote.

Waamuzi hao wa ligi ya ndani wataripoti na kujisajili Kituo cha Dar es Salaam Julai 29 na siku inayofuata Julai 30, 2016 na Julai 31, 2016 watakuwa na kozi ya kitathmini kasi kwa kukimbia kabla ya Agosti 1 na 2, 2016 kuwa na semina darasani na mitihani wakati Agosti 3, 2016 kutakuwa na semina na mitihani kwa makamishna mbalimbali wa michezo ya mpira wa miguu.
IMETOLEWA NA TFF