Saturday, July 16, 2016

UHAMISHO: N'GOLO KANTE ATUA STAMFORD BRIDGE!

KIUNGO wa France N'Golo Kante yupo njiani kujiunga na Chelsea kwa mujibu wa ripoti za ndani.
Kante, ambae alijiunga na Mabingwa wa England Leicester City Msimu uliopita akitokea Klabu ya Caen kwa Dau la Pauni Milioni 5.6, sasa atanunuliwa na Chelsea kwa kitita cha Pauni Milioni 29.

Kante, Kiungo Mkabaji aliechezea Leicester Mechi 38 Msimu uliopita akikosa Mechi 1 tu ya Ligi akiwabeba kutwaa ubingwa, pia aling’ara akiichezea Timu ya Taifa ya France kwenye Fainali za EURO 2016 zilizochezwa huko France hivi Juzi tu.

Mapema Wiki hii, Meneja wa Leicester, Claudio Ranieri, alisema Kante, mwenye Miaka 25, amepewa Mkataba mpya na ana matumaini atabaki kwao King Power Stadium.

Hata hivyo, zipo dalili kubwa Kante ataungana na Meneja mpya wa Chelsea kutoka Italy, Antonio Conte.

Ikiwa Kante atakamilisha Uhamisho, atakuwa Mchezaji wa Pili kusainiwa na Meneja mpya Conte baada ya mapema Mwezi huu kusainiwa Mfaransa mwingine kutoka Marseille Michy Batshuayi kwa Pauni Milioni 33.