Saturday, July 2, 2016

VICENTE DEL BOSQUE AJIUZULU KUIFUNDISHA SPAIN, NI BAADA YA KUFANYA VIBAYA EURO 2016

KOCHA wa Spain Vicente del Bosque amejiuzulu wadhifa wake baada ya Timu yake kutupwa nje ya EURO 2016 kwa mujibu wa Ripoti za Magazeti makubwa huko Spain.
Magazeti hayo, AS na MARCA, yameripoti kuwa Del Bosque alimjulisha Rais wa RFEF, Shirikisho la Soka la Spain, Angel Maria Villar, uamuzi wake tangu Juzi Jumanne ikiwa ni Siku moja baada ya Spain kufungwa 2-0 na Italy na kutolewa nje ya EURO 2016.
Rais huyo wa RFEF akamtaka Del Bosque asitangaze uamuzi huo mpaka hapo Julai 15 baada ya Kikao kikubwa cha RFEF.

Del Bosque, mwenye Miaka 65, aliiongoza Spain kutwaa Kombe la Dunia Mwaka 2010 na EURO 2012 lakini pia aliisimamia Spain ikifedheheshwa huko Brazil na kushindwa kutetea Taji lao ilipotupwa nje ya Fainali za Kombe la Dunia katika hatua za Makundi tu.
Mkataba wa Del Bosque, ambae aliwahi pia kuifundisha Real Madrid, unatakiwa kwisha baada ya EURO 2016.

Alipohojiwa mara tu baada ya kufungwa na Italy Juzi Jumanne kuhusu hatima yake, Del Bosque alijibu: “Hamna sababu ya kurudia rudia hili, nitaongea na Rais na kuamua nini bora kwa Timu ya Taifa!”