Friday, August 19, 2016

LEO MAN UNITED v SOUTHAMPTON, POGBA KUKARIBISHWA NDANI YA OLD TRAFFORD


BAADA ya Siku 94, Ligi Kuu England, EPL, inarejea tena Old Trafford wakati Manchester United chini ya Meneja mpya Jose Mourinho ikitaka ushindi wao wa pili mfululizo kwenye Msimu huu mpya kufuatia Wikiendi iliyopita kushinda Ugenini kwa kuichapa Bournemouth 3-1.

Man United wanaingia kwenye Mechi hii huku Kikosi chao kikizidi kuimarika kufuatia Mchezaji wao mpya Paul Pogba kuweza kucheza Mechi hii baada ya Kifungo cha Mechi 1 pamoja na Beki Chris Smalling nae kumaliza adhabu yake.

Pogba, mwenye Miaka 23 na ambae sasa ndie Mchezaji wa Bei Ghali Duniani kufuatia Dau la ununuzi wake kutoka Juventus, aliikosa Mechi ya kwanza ya Man United Wikiendi iliyokwisha akiwa Kifungoni Mechi 1 kutokana na Kadi za Njano 2 alizopata huko Italy Msimu uliopita.
Kufuatia Uhamisho wake kuchelewa kukamilika kutokana na kuwa Vakesheni iliyopitiliza kutokana na ushiriki wake kwenye EURO 2016 akiichezea Nchi yake France, Pogba amekuwa Mazoezini na Man United kwa Siku 11 tu.

Lakini Mourinho anaamini Pogba yuko tayari kucheza Mechi hii hata kama hatadumu Dakika 90.

Mourinho ameeleza: “Tulipocheza na Leicester walikuwepo Wachezaji ambao walikuwa na Mazoezi kidogo kupita Pogba.”

Akiongea na Wanahabari hapo Jana, Mourinho alieleza Pogba amefanya Mazoezi kwa Siku 11 na imekuwa rahisi kumbadili na kumuweka sawa kwa vile ni Kijana aliekulia Old Trafford na anamjua kila Mtu.