Saturday, August 6, 2016

MANJI ‘KUIKODI’ YANGA KWA MIAKA 10, MGAO FAIDA 75% KWAKE, 25% KLABU, HASARA YOTE YAKE!


MWENYEKITI wa Vigogo wa Soka Tanzania Yanga, Yusuf Manji, Leo amepitishwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Klabu hiyo kuikodi Yanga kwa Miaka 10 ili iendeshwe na Makampuni yake.
Mapema kwenye Mkutano huo uliofanyika Diamond Jubilee Hall Jijini Dar es Salaam, Wajumbe Watatu wa Kamati ya Utendaji walitimuliwa ambao ni Ayoub Nyenzi, Salum Mkemi na Hashim Abdallah.
Pia Mwanachama mmoja, Siza Lyimo, alinusurika baada ya kuomba radhi na kuruhusiwa kuendelea na Mkutano huo.

Kwenye Mkutano huo, Manji amesema ameomba kuikodisha Yanga kwa Miaka 10 na Mgao wa Faida ni Asilimia 75 kwake na 25 kubaki kwa Wanachama lakini ikiwa kuna Hasara basi yeye ndie ataibeba yote na si Klabu au Wanachama.

Manji amefafanua kuwa uendweshaji wa Klabu kwa mfumo huo utahusu Timu na Nembo tu wakati Majengo ya Klabu yanabakia kwa Wanachama.

Kwenye Mfumo huo, Manji amefafanua kuwa masuala yote ya Timu kuhusiana na Mishahara, Usajili, Safari na gharama nyingine zitakuwa upande wake. Wanachama wa Yanga waliridhia maombi hayo ya Manji na sasa mchakato utaendelea kuhusisha Bodi ya Wadhamini ili Makubaliano yasainiwe rasmi