Thursday, August 11, 2016

UHAMISHO: BEKI WA VALENCIA MUSTAFI AKUBALI KWENDA ARSENAL, KLABU ZAVUTANA ADA!

Arsenal na Valencia zipo kwenye mvutano mkubwa wa Ada ya Uhamisho wa Beki Shkodran Mustafi ingawa tayari Mchezaji huyo kutoka Germany ameshakubali kuhamia Arsenal.
Wakali wa Mustafi, Ali Bulut, ametoboa kuwa Beki huyo ashaafikiana na Arsenal kuhusu Maslahi yake binafsi na kilichobaki ni makubaliano kati ya Klabu hizo mbili.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger hivi sasa anahaha kuimarisha Difensi yake baada ya mapigo mawili ya kuumia Masentahafu wake Per Mertesacker na Gabriel ambao watakuwa nje kwa muda mrefu.

Sentahafu mwingine wa Arsenal, Laurent Koscielny, ndio kwanza tu ameanza mazoezi baada ya kurefusha Vakesheni yake kufuatia kuiwakilisha Nchi yake France kwenye EURO 2016 iliyomalizika Julai 10.

Ukimwondoa, Koscielny, Arsenal wamebakiwa na Masentahafu asilia Chipukizi Calum Chambers na Mchezaji mpya kutoka Bolton Wanderers, Rob Holding.
Valencia inamthamini Mustafi kwa Dau la Pauni Milioni 30 na alikuwemo Kikosi cha Mabingwa wa Dunia Germany waliofika Nusu Fainali ya EURO 2016.

Mustafi, mwenye Miaka 24, alianzia Soka lake huko Everton ya England kabla kuhamia Sampdoria ya Italy ambako aliuzwa kwa Valencia kwa Dau la Pauni Milioni 7 Mwaka 2014.