Friday, September 9, 2016

ANFIELD ‘MPYA - JUMAMOSI LIVERPOOL KUIFUNGUA NA MABINGWA LEICESTER!

LIVERPOOL watacheza Uwanja wa Nyumbani kwao Anfield Jumamosi kwa mara ya kwanza Msimu huu baada kucheza Mechi 3 za Ligi Kuu England, EPL, Ugenini wakipisha upanuzi wa Jukwaa Kuu la Uwanja wao.
Jumamosi Liverpool watawakaribisha Mabingwa Watetezi wa England Leicester City kwenye Mechi ya EPL ambayo itatanguliwa na Ufunguzi rasmi wa Jukwaa Kuu jipya ambao Mmiliki Mkuu wa Klabu hiyo kutoka Kampuni ya Kimarekani Fenway Group, John W Henry, Mwenyekiti Tom Werner na Rais Mike Gordon watahudhuria.

JE WAJUA?
-Kupanuliwa kwa Jukwaa Kuu la Anfield kutaiongezea Mapato Liverpool kwa Siku za Mechi kwa kiwango cha Pauni Milioni 20 hadi 30 kwa Msimu.
-Kabla, Liverpool walikuwa wakivuna Pauni Milioni 59 tu.
-Manchester United ndio wanaovuna kiwango cha juu kabisa cha zaidi ya Pauni Milioni 100.
Jukwaa hilo limepanuliwa na kuongezwa Ngazi 3 juu za kukalia Washabiki, kupanua Ukumbi wa Wachezaji kuingia na kutoka Uwanjani kutoka Vyumba vya Kubadili Jezi, Mabenchi ya Wachezaji wa Akiba na Jopo lao la Ufundi kutengenezwa upya, sehemu maalum kwa Walemavu na kuboreshwa kwa miundo mbinu ya Watazamaji.
Jukwaa Kuu la Anfield litaongeza Viti 8,500 na kuufanya Uwanja huo sasa upakie Watazamaji 54,000.