Tuesday, September 27, 2016

BIG SAM AACHIA NGAZI ENGLAND BAADA MECHI 1 NA SIKU 67 TU!

Sam Allardyce, maarufu kama Big Sam, ameacha kazi ya Umeneja wa Timu ya Taifa ya England baada ya kuwa Madarakani kwa Siku 67 tu na kusimamia Mechi 1 tu.
Kung’atuka huku, ambako kumesemwa ni kwa makubaliano ya pande mbili, kumekuja baada ya Gazeti la Uingereza The Daily Telegraph kudai alizungumzia njia zisizo halali za Uhamisho wa Wachezaji.
Gazeti hilo limechapisha habari kuwa Maripota waliojifanya Wafanyabiashara walizungumza na Allardyce na yeye alikiri inawezekana kuizunguka Sheria ya FA, Chama cha Soka England, ya Mwaka 2008 ya kuzuia Mchezaji kuwa Mali ya Mmiliki mwingine Kibiashara mbali ya Klabu yake.

Pia, ripoti ya Telegraph ilidai alimdhihaki Meneja wa England aliemrithi, Roy Hogson, huku pia akisema FA inajali kutengeneza Fedha tu.
Gazeti hilo pia lilirusha mtandaoni Video inayoonyesha Mkutano huo na Wafanyabiadhara feki wakati Big Sam akimponda Hodgson na kuikandya FA.
Vile vile, Gazeti hilo limedai Allardyce, mwenye Miaka 61, alitaka kutumia wadhifa wake ilia pate Dili ya kumwingizia Pauni 400,000 kwa kuiwakilisha Kampuni ya huko Mashariki ya Mbali Ya Asia.

FA imetamka kuwa Gareth Southgate atakaimu nafasi ya Umeneja wa England.