Tuesday, September 27, 2016

DAR DABI: YANGA PEMBA, SIMBA MORO, PLUIJM AISAHAU STAND, AIKAZIA SIMBA!

VIGOGO na Mahasimu wakubwa wa Soka Tanzania, Yanga na Simba, zimejikita kambini kujifua kwa mtanange wao wa Jumamosi Oktoba 1 ikiwa ni Mechi ya VPL, Ligi Kuu Vodacom.
Wakati Yanga, ambao ndio Mabingwa Watetezi wa VPL, wakijichimbia huko Visiwani Pemba, Simba wako Mjini Morogoro.
Wakati Simba iko shwari baada ya mafanikio yao yaliyowapaisha kileleni mwa VPL, Yanga ndio kwanza wanatoka kwenye kichapo cha kwanza Msimu huu cha Jumapili iliyopita walipofungwa huko Kambarage, Shinyanga 1-0 na Stand United kilichowaacha Nafasi ya 3 wakiwa na Pointi 10 kwa Mechi 5.
Simba wanaongoza VPL baada ya kucheza Mechi 6 na wana Pointi 16 wakifuata Stand United wenye Pointi 12 kwa Mechi 6.
Kisha Nafasi za 4 na 5 zipo Azam FC na Mtibwa Sugar zote zikiwa na Pointi 10 kila mmoja.
Katika kuelekea Dabi ya Dar es Salaam na watani zao Simba, Kocha wa Yanga kutoka Holland, Hans van der Pluijm, amesema watatoka kidedea kwenye mtanange huo licha kufungwa na Stand United kwenye Mechi iliyopita.
Pluijm amesema hawatamlaumu yeyote kwa kufungwa kwao na badala yake watarejea 'ubaoni' kurekebisha kasoro zao ndogo.
Msimu uliopita, kwenye VPL, Yanga iliichapa Simba nje ndani Bao 2-0 kila Mechi.
Pluijm pia ametoboa Kikosi chake kipo kamili bila Majeruhi.
Pluijm, ambae amekiri Simba ya sasa ni nzuri kupita Msimu uliopita, ameeleza: "Tumesahau kufungwa na Stand United na mkazo ni Simba. Ni wazi tutakuja na mbinu mpya kwa sababu ya Mechi yenyewe. Tuna kila sababu ya kuamini ushindi Wikiendi hii!"