Thursday, September 15, 2016

EUROPA LEAGUE: FEYENOORD ROTTERDAM 1 v 0 MANCHESTER UNITED, UNITED WAANZA KWA KICHAPO

BAO la Dakika ya 79 la Vilhena limewapa ushindi wa 1-0 Wenyeji Feyenoord dhidi ya Manchester United kwenye Mechi ya kundi A la UEFA EUROPA LIGI huko Uwanjani De Kuip, Stadion Feijenoord Jijini Rotterdam Nchini Netherlands.

Kwenye Mechi nyingine ya Kundi A kati ya Zorya Luhansk ya Ukraine na Fenerbahçe ya Uturuki iliisha 1-1.

Meneja wa Man United Jose Mourinho aliamua kupangua Kikosi chake cha kawaida kwa kuwapumzisha Wachezaji 8 na kubakisha Watatu tu, Kipa De Gea, Sentahafi Eric Bailly na Pogba, kwa kuwatumia Wachezaji ambao wamekuwa hawana namba Msimu huu.
Licha ya kutawala Mechi dhidi ya Wapinzani waliokamia na kutumia ubabe uliofumbiwa macho na Refa wa Spain Jesús Gil Manzano, Man United walishindwa kupenya Golini.

Dakika ya 73, Mourinho alifanya mabadiliko Matatu kwa mpigo kwa kuwatoa Marcus Rashford, Anthony Martial na Juan Mata na kuwaingiza Zlatan Ibrahimovic, Ashley Young na Memphis Depay.

Feyernoord, chini ya Kocha Giovanni van Bronckhorst aliekuwa Mchezaji wa zamani wa Arsenal, walipata Bao lao kinyume na mwenendo wa Gemu, waliponasa Mpira na kumpenyezea Nicolai Jorgensen, aliekuwa wazi Ofsaidi, kumpasia Tonny Vilhena aliefunga kilaini katika Dakika ya 79.

VIKOSI:
Feyenoord:
Jones, Karsdorp, Botteghin, Van der Hheijden, Kongolo, El Ahmadi, Kuyt, Vilhhena, Berghuis, Jorgensen, Toornstra
Akiba: Hansson, Woudenberg, Nieuwkoop, Vejinovic, apia, Basacikoglu, Kramer

Manchester United: De Gea, Darmian, Bailly, Smalling, Marcos Rojo, Schneiderlin, Ander Herrera, Mata, Pogba, Martial, Rashford
Akiba: Romero, Fosu-Mensah, Carrick, Fellaini, Memphis, Young, Ibrahimovic
REFA: Jesús Gil Manzano [Spain]