Tuesday, September 20, 2016

GUARDIOLA: ‘YAYA TOURE HATACHEZA TENA CITY KAMA WAKALA WAKE HAOMBI RADHI!’

WAKALA AJIBU: ‘NTAMWOMBA RADHI GUARDIOLA KAMA YEYE ATAMTAKA RADHI PELLEGRINI!’
Yaya Toure ameambiwa na Meneja Pep Guardiola kwamba hatachezea tena Manchester City mpaka Wakala wake atakapoomba radhi kwa matamshi yake kwenye Vyombo vya Habari.
Mara baada ya kauli hiyo, Wakala wa Toure, Dimitri Seluk, akajibu mapigo na kumtaka Guardiola ndie aombe radhi kwa Manuel Pellegrini na Kipa Joe Hart.
Kauli ya Seluk kwa Vyombo vya Habari iliyoleta tafrani hii ni pale alipodai Guardiola amemfedhehesha Toure kwa kumuacha kwenye Kikosi cha Man City cha UCL, UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu huu.
Tangu Guardiola atue City mwanzoni mwa Msimu huu, Toure amecheza Mechi 1 tu kati ya 8 City walizocheza hadi sasa.

Guardiola ameeleza kuwa ilikuwa ngumu kwake kumuacha Toure kwenye Kikosi cha UCL.

Guardiola akaongeza: “Lakini Siku Wakala wake alipoongea, hapo hapo Yaya alikuwa nje. Nitakubali tu arejee ikiwa Dimitri Seluk ataongea kwa Rafiki zake wa Vyombo vya Habari na aiombe radhi Man City, na Wachezaji wenzake na Kocha, na hilo likitokea Yaya atakurudi Kundini na atakuwa na nafasi kucheza Mechi zote kama wengine.”

Wachambuzi wengi wanaamini Guardiola hampendi Toure kwani ni yeye aliemuuza Mchezaji huyo wa Ivory Coast kwa Man City walipokuwa wote huko Spain Klabuni FC Barcelona.

Kauli hiyo ya Guardiola haikuchukua muda kwa Wakala Dimitri Seluk kujibu mapigo kwa kumponda Kocha huyo kutoka Spain.

Seluk amesema: “Nitaomba radhi kwa Guardiola akiomba radhi kwa Manuel Pellegrini!”

“Guardiola si muungwana, alisababisha Pellegrini aondolewe. Pellegrini ni muungwana. Guardiola pia anapaswa kumtaka radhi Joe Hart. Si sahihi kuja England na kuwatimua Wachezaji wachache wa Kiingereza waliokuwepo!”