Monday, September 19, 2016

KASEJA AACHA GUMZO IVORY COAST

Ivory Coast imeiondoa Tanzania katika mchezo wa mpira wa miguu wa ufukweni baada ya kushinda kwa mabao 6-4, lakini wamebaki na jina la Kipa Na. 1 wa timu ya Tanzania, Juma Kaseja wakisema: “Angekuwa tangu mwanzo, wangekuwa na wakati mgumu.”

Kaseja alikuwa kikwazo kwa Ivory Coast katika mchezo uliofanyika Jumamosi iliyopita huko jijini Abdijan ambako wenyeji walitamba kwamba wangeshinda mabao mengi, lakini kikwazo kilikuwa Kaseja na wakahoji wenyeji wa Tanzania: “Anacheza timu gani Tanzania, au mmemtoa nje ya nchi?”

“Kaseja alicheza kwa umahiri na kuzuia michomo mingi kutoka kwa washambuliaji wa Ivory Coast, na mabao aliyofungwa yalikuwa ni kwa bahati mbaya,” amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu mara baada ya kurejea kutua jijini Dar es Salaam leo alfajiri.

Tanzania imeondolewa kwa jumla ya mabao 13-7 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani kupoteza kwa mabao 7-3. Michezo hiyo ni ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni ambako fainali zake zitafanyika jijini Lagos, Nigeria Desemba, mwaka huu.

TFF imepanga kuhakikisha kwamba inaboresha soka la ufukweni baada ya kutengeneza uwanja maalumu wa mchezo huo ulioko kando ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

SERENGETI BOYS KUPIGA KAMBI NJE TENA
Baada ya kuifunga Congo-Brazzaville mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika, timu ya taifa Serengeti inatarajiwa kuondoka Alhamisi wiki hii kwenda kupiga kambi nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, taratibu zinapangwa kuhakikisha kwamba timu hiyo inakwenda kupiga kambi kwenye nchi tulivu inayolingana hali ya hewa na Congo Brazzaville kadhalika chakula pamoja na mazingira. Tanzania na Congo Brazzavile, zinatarajiwa kurudiana Oktoba 2, 2016 huko Congo Brazzaville na timu itakayopata ushindi wa jumla katika michezo miwili itafuzu kwa fainali hizo.

Katika mchezo uliofanyika jana Septemba 18, 2016 timu hiyo ya Tanzania maarufu kwa jina la Serengeti Boys ilipata mabao yake kupitia Yohana Mkomola na Abdi Makamba wakati yale ya Congo yalifungwa na Langa-Lesse Percy na Makouana Beni ambao mashabiki wa soka walikuwa wakiwalalamikia kuwa ni “wakubwa.”

Ili ifuzu kwa fainali zitakazofanyika mwakani huko Antananarivo, Madagascar katika fainali zitakazoanzia Aprili, 2017, Serengeti Boys inatakiwa ibaki na matokeo yake ya sasa na ihakikishe inapata ushindi na kama sare basi wapate bao kufuta faida ya bao la ugenini ambalo Congo Brazzaville walikuwa wanasheherekea baada ya mchezo.
IMETOLEWA NA TFF