Saturday, September 3, 2016

LIGI KUU ENGLAND - TUZO YA UBORA AGOSTI: WAGOMBEA MAMENEJA, WACHEZAJI WATAJWA, NI WALE WA TOP 4"

LISTI ya Wagombea wa Tuzo za Ubora kwenye Ligi Kuu England, EPL, kwa Mwezi Agosti imetangazwa na safari hii Mashabiki nao watachangia kwenye Kura kwa kutumia Mtandao wa Twitter.
Msimu uliopita Tuzo za Meneja Bora na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England zilikuwa zikiamuliwa na Wadhamini wa Ligi hiyo, Barclays, lakini safari hii Ligi hii haina Mdhamini na hivyo uamuzi utatolewa na Jopo Maalum la EPL kwa kuchukua pia Kura za Wadau zitakazopigwa kwenye Mtandao wa Twitter.
Walioteuliwa kugombea Tuzo ya Meneja Bora kwa Mwezi Agosti ni Jose Mourinho wa Man United, Pep Guardiola wa Man City, Antonio Conte wa Chelsea ambao Timu zao ndio pekee zilizoshinda Mechi zao zote 3 za kwanza za EPL pamoja na wa Hull City ambae ni Meneja wa muda Mike Phelan anaeongoza Timu ambayo si Kigogo na ipo mashakani kutokana na umiliki wake.

Kwa upande wa Wachezaji Wagombea ni Antonio Valencia wa Man United, Curtis Davies (Hull), Eden Hazard (Chelsea) na Raheem Sterling (Manchester City).
Upigaji Kura kwa Wagombea utafungwa Saa 8 Usiku, Saa za Bongo, Septemba 6.