Thursday, September 29, 2016

MARCUS RASHFORD ATEGEMEWA KUITWA ENGLAND BAADA KUACHWA KIKOSI CHA U-21!


Marcus Rashford anatarajiwa kuitwa kuchezea Kikosi cha Kwanza cha England wakati Meneja Mpya wa Muda Gareth Southgate akitangaza Kikosi chake kwa mara ya kwanza kabisa baada ya Chipukizi huyo wa Manchester United kutotajwa katika Kikosi cha England U-21.
Aidy Boothroyd, alieshika wadhifa wa Kocha Mkuu wa England U-21 akichukua nafasi ya Southgate, amemwacha Rashford kwenye U-21 ambayo itawavaa Kazakhstan na Bosnia & Herzegovina kwenye Mechi za Mchujo kucheza Fainali za U-21 EURO 2017 Wiki ijayo.

Southgate ameteuliwa Juzi kuwa Meneja wa Muda wa England baada ya Sam Allardyce kuachia ngazi na Jumapili hii anatarajiwa kutangaza Kikosi cha kuzivaa Malta na Slovenia za Kundi lao za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.

Rashford, ambae alikuwemo Kikosi cha England kilichocheza Fainali za EURO 2016 huko France Mwezi Juni na Julai, hakuitwa kuichezea Mechi iliyopita ya England chini ya Sam Allardyce walipoifunga kwa mbinde Slovakia 1-0 kwenye Mechi ya Kundi lao la kufuzu Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 na badala yake akaitwa kuichezea U-21 dhidi ya Norway waliyoitwanga 6-1 huku Rashford akipiga Hetitriki.

Rashford, mwenye Miaka 18 na alieanza kuichezea Timu ya Kwanza ya Man United mwishoni mwa Msimu uliopita, aliichezea kwa mara ya kwanza Timu ya Kwanza ya England Mei 27 kwenye Mechi ya Kirafiki na Australia na kupiga Bao Dakika 3 tu baada kuingizwa na kuweka Historia ya kuwa Mchezaji wa Kwanza kabisa wa England mwenye Umri mdogo kupachika Bao katika Mechi yake ya kwanza kabisa.