Saturday, September 24, 2016

MOURINHO AKANUSHA NUKUU YA ‘KUBOMOA SURA YA WENGER’!

Jose Mourinho amesema hana tatizo na Arsene Wenger licha ya kuchapishwa Kitabu kikimnukuu yeye akisema ‘ataibomoa Sura ya Wenger’.
Mourinho, ambae sasa ni Meneja wa Manchester United, amekuwa na upinzani wa muda mrefu na Wenger ambae ni Meneja wa Arsenal na hasa wakati Mourinho akiwa ni Meneja wa Chelsea.
Akiwa huko Chelsea, Mourinho aliwahi kumbatiza Wenger kuwa ni ‘Spesho wa Kushindwa’.

Nukuu hiyo ya kwamba ‘ataibomoa Sura ya Wenger’ ipo kwenye Kitabu kiitwacho Jose Mourinho: Up Close and Personal kilichaoandikwa na Mwanahabari Rob Beasley.

Jana, Wenger alipogusiwa kuhusu Kitabu hicho alisema hatakisoma.
Na Jana hiyo hiyo, Mourinho akaulizwa kuhusu Kitabu hicho na kujibu: “Utaona yuko karibu na mimi. Nina furaha. Ametengeneza Pesa zake, hilo sawa kwangu!”

Mourinho aliongeza: "Nilikutana na Arsene Wenger Wiki chache zilizopita, na kama Watu wastaarabu, tukapeana mikono. Tukakaa Meza moja na kula Chakula cha Usiku pamoja na Watu wengine. Tukabadilishana mawazo, tuliongea kwa sababu sisi ni Watu tuliostaarabika. Kwa mara nyingine sidhani Kitabu hiki kitakaa Maktaba moja na vile vya Shakespeares na vingine!”

Aliongeza: “Sitaongeza lolote jingine. Hilo ni neno langu la mwisho. Narudia huyo ametengeneza Pesa yake. Hilo sawa kwangu!”