Sunday, September 25, 2016

MOURINHO - 'ROONEY BADO MCHEZAJI MKUBWA MAN UNITED'!

MENEJA wa Manchester United Jose Mourinho amepasua kuwa Wayne Rooney bado ni Mchezaji mkubwa kwa Timu yao.
Mourinho amesema ana imani yote kwa Rooney na kuamini kuwa Kepteni huyo wa Manchester United bado ni Mchezaji muhimu kwa Timu yao licha ya jana kumuanzisha Benchi wakati wakiwafunga Mabingwa wa England Leicester City 4-1 Uwanjani Old Trafford kwenye Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Rooney kutoanza Mechi chini ya Mourinho na mara ya mwisho kwa Kepteni huyo kupigwa Benchi ni Desemba 26 Mwaka Jana.
Mourinho ameeleza: "Ni Mtu wangu, namuamini kwa kila kitu. Yeye ana furaha kama mimi na hii ndiyo Timu."
Aliongeza: "Yeye ni Mchezaji mkubwa kwangu mimi, United, Mchezaji mkubwa kwa Nchi hii!"

Hapo Jana, bila Rooney kuwemo Uwanjani, Man United ilibamiza Bao 4 Kipindi cha Kwanza kwa Bao za Chris Smalling, Juan Mata, Marcus Rashford na Paul Pogba.

Garth Crooks (Mchambuzi aliechezea England, Stoke, Spurs, Man United, WBA, Charlton Athletic):
"Wayne Rooney bado ana mchango mkubwa kwa Manchester United na hafai kuwekwa Benchi. Ana mchango mkubwa kwa Man United na England kama Kepteni wao!"

Mourinho alimwingiza Rooney kwenye Mechi hiyo zikibaki Dakika 7 Mpira kwisha.
Akisakamwa na Maswali ya Wanahabari baada ya Mechi hiyo na Leicester, Mourinho alijibu: "Kama sikumchezesha Rashford mnauliza kwanini, kama hakucheza Jesse Lingard mnauliza kwa nini na Siku zote mnapenda kuhoji kwanini fulani hachezi."
"Mara nyingine nikisoma habari zenu, najiona kama sijui chochote kuhusu Soka."
"Lakini kuna kitu kimoja nakijua na hicho ni Sheria za Soka kwamba natakiwa kuanza na Wachezaji 11. Mpaka aje Mtu kunieleza kuna mabadiliko naweza kuanza na Wachezaji 11 tu!"