Friday, September 23, 2016

PATASHIKA JUMAMOSI OLD TRAFFORD MAN UNITED vs LEICESTER, RANIERI ADAI BIFU NA MOURINHO LIMEKUFA!

MABINGWA wa EPL, Ligi Kuu England, Leicester City Mchana Jumamosi wapo Old Trafford kuivaa Manchester United na Meneja wao Claudio Ranieri amesema hana tena bifu na Jose Mourinho.
Huko nyuma, Ranieri na Mourinho waliwahi kukwaruzana hasa baada ya Mourinho kutua Chelsea kumbadili Ranieri.

Lakini Jana, akihojiwa na Wanahabari kuelekea Mechi yao ya Jumamosi, Ranieri alieleza: “Mourinho ni Meneja Bora sana, mjanja na mwerevu sana. Ishu yetu ilikuwa zamani sana!”

Mourinho alimbadili Ranieri huko Chelsea Mwaka 2004 na kudai Klabu hiyo ilimuona Mtaliana huyo ni ‘Mtu mwenye chuki ya kushindwa’!
Wawili hao walikumbana uso kwa uso huko Italy na kukwaruzana mara kwa mara wakati Ranieri akiziongoza Juventus na AS Roma na Mourinho kuwa na Inter Milan iliyotwaa Trebo, yaani, UEFA CHAMPIONS LIGI, Ubingwa wa Serie A na Coppa Italia, Mwaka 2010.

Lakini Ranieri amedai bifu hilo limepitwa na wakati.
Amenena: “Uhusiano wetu ni mzuri. Hatuna tatizo. Akinipa Ofa ya Mvinyo Mwekundu ninaoupenda baada ya Mechi nitaenda kunywa!”
Wawili hawa walivaana uso kwa uso Uwanjani Wembley Jijini London Mwezi Agosti na Mourinho kuibuka kidedea baada ya kuitwanga Leicester ya Ranieri 2-1 na kutwaa Ngao ya Jamii.